18 September 2012

Vita ya Ubunge CCM 2015 yaanza *Pindi Chana adaiwa kumvaa Filikunjombe


Na Mwandishi Wetu, Ludewa

VITA ya ubunge Jimbo la Ludewa, mkoani Njombe, kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao 2015, imeanza kujionesha wazi baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Pindi Chana, kudaiwa kufanya jitihada za kumpigia debe mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa UWT, wilayani humo.


Baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM jimboni humo, wanadai jitihada za Bw. Chana kumpigia debe mgombea huyo ni maandalizi ya kunyakua jimbo hilo ambalo hivi sasa lipo chini ya mbunge wake Bw. Deo Filikunjombe.

Hata hivyo, mgombea aliyekuwa akipigiwa debe na Bw. Chana, alianguka vibaya katika uchaguzi huo na yule aliyekuwa akiungwa mkono na Bw. Filikunjombe, alipata ushindi wa kishindo.

Chanzo chetu cha habari kimelidokeza gazeti hili kuwa, kutokana na sakata hilo, viongozi wa juu wa CCM Mkoa wa Njombe na Iringa, walilazimika kufika wilayani Ludewa ili kusimamia uchaguzi huo badaa ya kubaini ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu.

Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa ambaye pia anashikilia Mkoa wa Njombe, Bw. Deo Sanga, alithibitisha kutokea kwa tafrani ya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi huo na kudai kuwa, wao kama viongozi wa chama walisimama kidete kuhakikisha misingi na taratibu za chama zinafuatwa.

Inaelezwa kuwa, chanzo cha mgogoro huo ni Bw. Chana kufanya kampeni ya kuhakikisha mgombea wake Bi. Anna Mlowe, anashinda nafasi hiyo Bi. Mary Mapunda, ambaye alikuwa akiungwa mkono na Bw. Filikunjombe, anaanguka.

Hata hivyo, katika uchaguzi huo Bi. Mapunda aliibuka kidedea kwa kupata kura 274, wakati Bi. Mlowe akipata 108 na mshindi wa tatu alikuwa Bi. Selina Haule ambaye aliambulia kura 14.

“Sisi viongozi tunajua wazi kwamba Bw. Chana ana mpango wa kutaka kugombea jimbo hili lakini bado anakabiliwa na upinzani mkali na Bw. Filikunjombe ambaye anakubalika sana.

“Kiini cha mvutano uliojitokeza juzi katika uchaguzi huu ni baada ya Bw. Chana kutaka kupanga watu wake ili wajijengee mazingira mazuri ya ushindi kkatika Uchaguzi Mkuu ujao.

“Kama unavyojua mwandishi viongozi wa jumuiya za chama kama UVCCM (Umoja wa Vijana wa CCM), UWT na Jumuiya ya Wazazi wakiwa upande wako ni rahisi kushinda,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa, mgogoro mkubwa ulizuka baada ya jina la Bi. Mapunda, kutoonekana katika fomu ya kupigia kura huku wakati jina la Bi. Mlowe likiwepo.

“Tulishangaa kuona jina la mgombea wetu (Mapunda) halipo lakini la (Mlowe), lipo pamoja na wagombea wengine, kutokana na utata huu, Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Njombe, iliamua kuwatuma viongozi wake akiwemo Bw. Sanga na Katibu wa chama hicho Mkoa wa Njombe, Bw. Hoseah Mpagike kwenda Ludewa kuhakiki mwenendo wa uchaguzi huo.

“Viongozi hawa walipofika walibaini kuwepo kasoro katika ujazaji fomu za muhtasari kwa wagombea hivyo waliagiza marekebisho yafanywe na majina ya wagombea kutathminiwa upya na ndipo uchaguzi ufanyike ambapo Bi. Mapunda aliibuka kidedea,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, mshindi wa nafasi hiyo Bi. Mapunda, alidai Bw. Chana amemdhalilisha kwa kumtolea lugha ya matusi.

“Kwa kweli amenitukana sana na pale kulikuwa na watu wa rika zote kuanzia wakina mama, watoto na wanaume, sijajua kwanini aliamua kufanya vile wakati yeye ni kiongozi anayeheshimika.

“Binafsi nilishiriki kumpigia kura nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Wilaya,” alisema Mapunda.

Kutokana na sakata hilo, gazeti hili lilimtafuta Bw. Chana, ambaye alikiri kutokea kwa vuta nikuvute katika uchaguzi huo lakini alikataa kulizungumza kwa undani na kudai linafanyiwa kazi na chama.

“Hivi sasa nipo kikaoni lakini naweza kukupigia nitakapokuwa katika nafasi nzuri ya kulielezea kwa kina,” alidai Bw. Chana lakini hadi jana hakuweza kupiga simu kulizungumzia suala hilo.

Kwa upande wake, Bw. Filikunjombe alikiri kuwepo kwa taflani hiyo na kudai kuwa, haukuwa mgogoro kati yake na Bw. Chana bali ulihusisha kwa kiasi kikubwa wagombea wa kiti hicho.

“Si kwamba tulizozana ana kwa ana na Bw. Chana hapana,  Kilichotokea ni kwamba mwenzangu alikuwa na mgombea anayemuunga mkono na akina mama wa Ludewa walikuwa na mgombea wao.

“Yeye alitaka kutumia nguvu kama Mjumbe wa Kamati Kuu kupindisha sheria ili mgombea wake ashinde, lakini sisi tulisimama kidete kuhakikisha kanuni za chama zinazingatiwa kumpata mshindi halali.

“Kwa mfano, alama alizowekewa Bi. Mlowe hakuna kikao chochote kuanzia Kamati ya Utekelezaji ya Wanawake Wilaya, Baraza la Wanawake Wilaya na Kamati ya Siasa Wilaya waliohusika kuziweka, Bw. Chana alitaka haya yote yapuuzwe na viongozi walipomweleza yeye akaleta ubabe,” alisema Bw. Filikunjombe.

Kwa upande wake Bw. Sanga, alisema suala hilo limepatiwa ufumbuzi baada ya kurekebishwa kasoro zilizojitokeza.

“Sisi tulikwenda kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa kufuata misingi na taratibu za chama chetu baada ya Halmashauri ya Mkoa kutuagiza twende kulishughulikia kutokana na utata uliokuwepo.

“Hapa ninapozungumza na wewe uchaguzi umeshafanyika na mshindi halali Bi. Mapunda,” alisema Bw. Sanga.

1 comment:

  1. Wewe mwandishi, Pindi Chana ni Mwanamke, wewe wamwita Bw, kulikoni?

    ReplyDelete