25 September 2012
'Viongozi Ilala toeni elimu ya mazingira'
Na Willbroad Mathias
VIONGOZI na Watendaji wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, wametakiwa kutoa elimu ya mazingira kwa jamii na kuhamasisha suala zima la usafi.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Raymond Mushi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua warsha ya siku tatu iliyoshirikisha viongozi hao ili kupanga mikakati ya kuboresha mazingira katika manispaa hiyo.
Alisema kazi iliyopo mbele yao ni ngumu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kuhakikisha kanuni zinafuatwa ambazo ni malengo, mipango, kujiamini, kufahamu sababu ya kuwema miji katika hali ya usafi, kujituma na kusheherekea mafanikio.
“Kanuni hizi zina umuhimu mkubwa na kama zitafuatwa hatua kwa hatua, lazima mafanikio yatapatikana,” alisema Bw. Mushi.
Awali Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Bw. Khery Kessy, alisema manispaa hiyo inajitahidi kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira safi lakini bado kuna changamoto nyingi.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni wingi wa watu wanaoingia kila siku ndani ya manispaa hiyo, viongozi kutoshiriki kikamilifu kuhamasisha usafi na vitendea kazi vichache ukilinganisha na kiwango cha taka kinachozalishwa.
“Umefika wakati wa viongozi kushiriki kikamilifu kuhamasisha jamii ilinde mazingira,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment