24 September 2012

Utamaduni wa takrima katika chaguzi CCM tuukatae utatuumiza



HIVI karibuni, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza chaguzi zake katika ngazi mbalimbali ili kupata viongozi waadilifu ambao watakiwezesha chama hicho kitekeleze ilani zake kwa vitendo.

Baadhi ya wagombea waliochukua fomu wanaamini kuwa, uwezo wao kiutendaji katika nafasi walizoomba kugombea, ndio nguzo ambayo itawawezesha kuibuka na ushindi.

Chaguzi hizo zinapewa umuhimu mkubwa kutokana na ukweli kwamba, ndio sehemu ya maandalizi ya CCM kuendelea kushika dola katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Rais Kkwete aliwahi kusema kuwa, Serikali yake haipo tayari kuona uongozi ndani ya chama hicho unanunuliwa kama njugu au shati.

Haya ni maneno mazito ambayo aliyasema Rais Kikwete wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mwaka 2011, jijini Mwanza.

Alisema rushwa katika uchaguzi ni tatizo kubwa na kama hatua za dhati hazitachukuliwa, Taifa litaangamia kwani kutoa na kupokea rushwa, inaonekana ni utaratibu wa kawaida.

Hivi sasa, matokeo ya maneno hayo tumeanza kuyashuhudia katika baadhi ya chaguzi zinazoendelea kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Wapambe wa wagombea wamekuwa wakipigana vikumbo ili kuhakikisha mgombea wake anashinda na pale anapokosa nafasi hiyo ndio mwanzo wana CCM kukosa umoja na mshikamano.

Sisi tunasema kuwa, kama wanachama CCM watazingatia kauli ya Rais Kikwete, wataweza kubadili mitazamo ya baadhi ya wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa, wameathiriwa na utaratibu wa takrima ambao umepigwa marufuku.

Kimsingi wanasiasa bado wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanaichukia rushwa kutoka ndani ya nafsi zao bila kushinikizwa.

Imani yetu ni kwamba, rushwa ndani ya uchaguzi inachangiwa na wanasiasa matajiri na wafanyabiashara ambao wanaamini siasa kwao ni zaidi ya uongozi.

Tuikatae rushwa kutokana na madhara yake ndio maana Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kwani inaathiri maendeleo ya mtu binafsi, familia, Taifa, kushusha hadhi ya mtoaji na mpokeaji.

Vitendo hivyo vinajumuisha matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha baadhi ya viongozi wa umma na sekta binafsi, kutumia madaraka waliyonayo kinyume cha sheria ili kujinufaisha.

Tukichagua viongozi wanaotoa rushwa, tutawanyima wananchi mategemeo ya kuwa na maisha bora, kuwakosesha elimu, huduma bora za afya, chakula, maji na mahitaji mengine ya kibinadamu.

No comments:

Post a Comment