06 September 2012
Simba, Sofapaka kukunjua makucha leo
Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba, leo inashuka uwanjani kuumana na SOFAPAKA ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
.
Katika mechi hiyo, mashabiki wa timu hiyo wasubiri kwa hamu kubwa kuwaona wachezaji wapya, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Okuffor.
Wachezaji hao wameonekana kuonesha kiwango kizuri katika mechi zao za kirafiki zilizochezwa jijini Arusha dhidi ya timu za Sony ya Kenya na JKT Oljoro, ambao leo itakuwa ni mara yao ya kwanza kucheza Dar es Salaam.
Akizungumzia mechi hiyo Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema timu yake inaendelea vizuri na mazoezi na kwamba jana asubuhi walifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Sigara jijini.
"Timu ipo vizuri na hatuna mchezaji majeruhi zaidi ya Felix Sunzu, ambaye amekwenda nyumbani kwao baada ya kufiwa pamoja na Emmanuel Okwi, ambaye yupo na timu ya Taifa ya Uganda, tuna imani timu hiyo ni kipimo kizuri kwetu," alisema Kamwaga.
Alisema mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwao kwani baada ya hiyo, watacheza na Azam FC katika Ngao ya Jamii Jumanne na mwishoni mwa wiki Ligi Kuu Bara itakuwa imeshaanza.
Aliwaomba mashabiki wao kujitokeza kwa wingi katika mechi hiyo kushuhudia viwango vya wachezaji wapya, kwani alitamba kazi waliyoifanya Arusha, wanataka kuionesha Uwanja wa Taifa.
Akizungumzia kurudi kwa Sunzu, alisema wanatarajia baada ya kumaliza shughuli iliyompeleka atarejea nchini kuendelea na majukumu yake kama kawaida, kwani wamempa siku 10 lakini kama kutatokea kitu kingine atatoa taarifa.
Kwa upande wake Okwi, alisema wana imani baada ya kumalizika mechi yao dhidi ya Zambia, atajiunga na wenzake kwani mashabiki wana kiu kubwa ya kumuona nyota huyo akiichezea tena timu hiyo.
"Tunamuhitaji Okwi, awepo katika mechi ya Ngao ya Jamii na tutahakikisha hilo linafanyika kwa wakati, kwani ni mechi ngumu kwetu na tunahitaji tuwe na kikosi kilichokamilika katika mechi hiyo," alisema.
Alisema mechi hiyo itapigwa Jumamosi mjini Ndola, Zambia na baada ya kumalizika siku itakayofuata wanatarajia ataanza safari ya kurejea nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment