06 September 2012

Sakata la Yondan, Twite Simba yaizulia mapya Yanga



Na Elizabeth Mayemba

UONGOZI wa Simba, umesema kutokana na watani Wao Yanga kuonesha jeuri ya kumsajili, Kelvin Yondan bila kufanya nao mazungumzo, sasa wanataka watani zao hao kuwalipa sh. milioni 60 ili mchezaji huyo aendelee kuwatumikia.

Kinyume na hapo Simba imesema, utaliaacha suala hilo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake, kwani kanuni zipo wazi kwamba anaweza kufungiwa miaka miwili kucheza soka kwa kuwa amejisajili katika klabu mbili.

Hatua hiyo ya Simba imefikiwa kikao cha juzi kati yao, Yanga na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa kushindwa kufikia makubaliano.

Katika kikao hicho kilichoanza saa saba mchana, hoja ya kwanza ilikuwa ni suala la Mbuyu Twite kuwachukua fedha Simba dola za Marekani 30,000 na dola 2,000 za kujikimu mchezaji huyo, lakini baadaye akasaini Yanga.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba Hans Pope, alisema suala la Yondan ni jepesi mno ambalo Yanga, wanatakiwa walipe sh. milioni 60 na kisha watamuachia beki huyo kwa kuwa ameonesha mapenzi na klabu hiyo.

"Awali tulitoa ofa ndogo sana kwa Yanga lakini wakaleta jeuri, sasa wakitaka tukae meza moja juu ya Yondan watulipe kiasi hicho, ili tumuachie ila kama wakiona hawawezi basi kwa mujibu wa sheria anatakiwa afungiwe kwa kuwa amesaini katika klabu mbili na wakizidi kuchelewa tutawapandishia dau," alisema Hans Pope.

Alisema pia katika kifungu cha 49 cha katiba, kinasema anayepaswa kutoa taarifa za kumaliza mkataba wa mchezaji ni klabu na si Shirikisho TFF, kwani klabu ndiyo inayofanya mazungumzo na mchezaji husika.

Katika suala la Twite, Mwenyekiti huyo amewataka Yanga wawakabidhi mchezaji huyo, ili wamalizane naye na kisha wamuachie kwani walipopeana fedha, Yanga hawakuwepo.

Hans Pope alisema Twite alisaini mkataba wa kuichezea timu yake mbele ya viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na Klabu ya APR na kisha wakamlipa dola za Marekani 30,000 na nyingine 2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga nao.



No comments:

Post a Comment