19 September 2012

Mgeja kuigawa CCM Shinyanga *Mpango wa 'kumtosa' asigombee wabainika



Na Suleiman Abeid, Shinyanga

HOFU ya kutokea mgawanyiko miongoni mwa wana CCM mkoani Shinyanga, imewakumba baadhi ya wanachama na wazee baada ya kuwepo fununu za jina la aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa, Bw. Khamis Mgeja, kutaka liondolewe ili asitetea nafasi hiyo.

Inadaiwa kuwa, mpango wa kuondoa jina lake ni shinikizo la baadhi ya vigogo ndani ya CCM ambao wanafanya kila jitihada kuhakikisha jina la Bw. Mgeja, linakatwa katika vikao vya mwisho kwa madai ya kutoliunga mkono kundi lao ambalo linajipanga kwa urais 2015.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kutoka kwa baadhi ya wana CCM mkoani hapa, kinadai hofu ya vigogo hao kama Bw. Mgeja atachaguliwa katika nafasi hiyo, atakuwa kikwazo cha kufanikisha mipango ya kumuandaa mtu wao kwa ajili ya urais.

Baadhi ya wazee ambao walizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, waliwataja vigogo hao (majina yanahifadhiwa), ambao ndio wanahusika kuhakikisha jina la Bw. Mgeja linaondolewa ili asiweze kutetea nafasi yake.

Inaelezwa kuwa, mkakati wa vigogo hao unaungwa mkono na baadhi ya wabunge wa CCM mkoani hapa ambao wanampiga vita Bw. Mgeja na kufanya vikao vya siri ili kufanikisha dhamira yao.

Katika hatua nyingine, mwanachama mmoja wa CCM mkoani hapa  ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema ili vigogo hao waweze kufanikisha lengo hilo, waliwahi kumshawishi kigogo mmoja wa chama hicho achukue fomu za kugombea nafasi hiyo  kwa lengo la kumrithi Bw. Mgeja.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, mmoja wa wagombea ambaye alipata fununu za jina lake kuwa miongoni mwa waliopendekezwa na vikao vya CCM Mkoa kugombea nafasi hiyo hivi karibuni alikesha katika hoteli moja eneo la Lubaga mjini hapa akifanya sherehe yeye na kambi inayomuunga mkono.

Zipo taarifa za kuwepo mawakala wa vigogo hao kuonekana katika maeneo tofauti wakikutana na baadhi ya wajumbe wa mkutano Mkuu wa CCM wa Mkoa ili kuwashawishi wasimpigie kura Bw. Mgeja kaama itatokea jina lake limerejeshwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC).

“Kila siku wana CCM tunaombwa tudumishe ushirikiano na mshikamano miongoni mwetu, leo viongozi wetu wanafanya kampeni chafu ambazo zitasababisha tugawanyike.

“Hakuna sababu ya watu kuanza kumuandaa Rais mtarajiwa 2015, hivi sasa tuna mengi ya kufanya badala ya kulumbana sisi kwa sisi hivyo ni bora demokrasia ikaachiwa ichukue mkondo wake,” alisema mwanachama wa CCM, Bi. Saada Jumanne.

Kwa upande wake, mmoja wa wazee wa CCM mjini hapa, Bw. Juma Amani, alishauri ni vyema vikao vya uteuzi vikatumia busara ili kuepuka mgawanyiko ambao utasababishwa na maamuzi yao

No comments:

Post a Comment