05 September 2012
Mazingira ya sekondari vijijini kikwazo maendeleo ya elimu
Na Juliana John
MAZINGIRA magumu ya kazi pamoja na maslahi duni ni mambo yanayotajwa zaidi kuwavunja moyo walimu wengi nchini hususan wanaofundisha za Sekondari za Kata.
Kumekuwa na ongezeko la shule nyingi katika miaka mitano, huku idadi ya walimu kushindwa kukidhi mahitaji.
Walimu wa masomo ya sayansi ni wachache hali inayotishia kukosekana kwa wataalamu hao miaka ijayo.
Ili kujenga kizazi kitakachoweza kujitegemea na kupambana na maisha ni vema serikali ikajikita zaidi katika kuzalisha walimu vijana ambao pia watafundishwa mbinu za kuwawezesha wanafunzi pindi watakapohitimu wajue jinsi ya kujitegemea.
Kinachoendelea sasa kuua masomo ya sayansi kwa sababu wahitimu wengi ni masomo ya art na kufanya idadi kubwa ya walimu mashuleni kuwa wa masomo hayo tofauti na walimu wa sayansi.
Je kulifanyika utafiti wa kutosha kabla ya kutekeleza azimio la shule za hizo? Je kwanini tulinuia zaidi kuongeza shule kabla ya kufanya maandalizi ya kuongeza wataalamu?
Tusingeweza kutumia fedha hizi kujenga shule chache na fedha nyingine kuboreshea mazingira ya kazi na vifaa vya kufundishia?
Lakini ipi mikakati ya viongozi wa shule hizi kuinua ari ya walimu kufanya kazi huku wakitambua kuwa baadhi ya walimu wamevunjika moyo?
Kimsingi ufundishaji katika shule nyingi umeshuka kwani utafiti uliofanywa na Shirika la HakiElimu mwaka jana ulibaini kwamba walimu wengi hawana ari ya kufundisha kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwamo mishahara midogo na kucheleweshewa malimbikizo, ukosefu wa nyumba za kuishi, barabara mbovu na maji.
Mkuu wa Sekondari ya Makanya mkoani Kilimanjaro Bw.Msami Mmbaga anasema kuwa “mara kwa mara tumekuwa tukishirikiana na walimu kufuatilia maslahi na stahili zao kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya na Chama cha Walimu kuhakikisha kila taarifa inayopatikana katika ufuatiliaji wanajulishwa”.
"Hiyo imetusaidia sana, tukifanikiwa wote tunafurahi na tukikwama walimu wanakuwa wanafahamu majibu tuliyopewa, tunaendelea kusubiri huku tukiendelea na ufuatiliaji kwa pamoja," anasema Bw.Mmbaga.
Aliendelea kisisitiza kuwa wamefanikiwa kupunguza malalamiko kutoka kwa walimu na wao kuona kwamba uongozi wa shule unatambua hoja zao.
Tatizo hili lisipofanyiwa kazi tutaendelea kuzalisha wataalamu wasioweza kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Sababu nyingine zinazochangia wanafunzi hao kufanya vibaya ni kujiunga kuanza masomo yao huku wakiwa hawana vigezo vya kuanza shule.
“Wanafunzi wengi tulionao hawajafikia vigezo vya kujiunga na elimu ya Sekondari, mfano kwa baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hawajui kusoma na matokeo ya kidato cha nne hayakuwa mazuri sana kwani tuna aina ileile ya wanafunzi ambao hawakuchujwa wakiwa kidato cha pili”.
Mtihani wa kidato cha pili ni muhimu kwa sasa na kwa kuwa umerudishwa basi watakaofikia kidato cha nne wataweza kufaulu wengi.
Je shule hizi zitaendelea hivi mpaka lini? Bila shaka wanafunzi walioko katika shule hizo kama ilivyo kwa wengine wanastahili elimu bora, kupata msingi na maarifa yatakayowasaidia maishani.
Yote hayo yanawezekana endapo tu maktaba zitaboreshwa kwa kuwa na vitabu vya kutosha, kujengwa kwa maabara na vifaa vya kufundishia pia kuongezwa kwa walimu kulingana na idadi ya wanafunzi ili kuweza kufikia malengo.
Wazazi pia wanaposhirikishwa kufahamu mipango ya maendeleo ya shule kwa ajili ya watoto wao ni jambo zuri katika kufanikisha nia ya wanafunzi kuwapo shuleni kwani ushirikiano baina yao unahitajika," anasema.
Hata hivyo utafiti uliofanywa na TAMWA ulilenga kuliwezesha Taifa kubaini mambo yanayochangia wanafunzi wa Sekondari za Kata kufeli na wengine kukutisha masomo.
Baada ya utafaiti huo Wakuu wa Wilaya wameshauriwa kuendeleza mikakati ya kuondoa matatizo yanayochangia wanafunzi wa Shule hizo za Kata kufeli na wasichana wengi kukatishwa masomo kutokana na kupata mimba au kulazimishwa kuolewa.
Kuthibitisha hayo, mwaka jana, Sekondari Nusuri Wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma yenye wanafunzi 691, wanafunzi 26 walipata mimba na kukatisha masomo, Shinyanga pia mwaka huohuo wanafunzi 51 walipata mimba wakati Tabora wanafunzi 41 nao walikutwa na janga hilohilo.
Wilaya zingine zilizohusishwa katika utafiti huo kwa Tanzania Bara ni Kilindi (Tanga), Bahi (Dodoma), Kisarawe(Pwani), Rombo(Kilimanjaro), Muleba(Kagera), Sengerema(Mwanza) na Kiteto(Manyara).
Licha ya matokeo hayo, lengo kubwa la Serikali ni kumkomboa mwananchi mwenye kipato cha chini kuweza kumsomesha mwanae kutokana na shule za watu binafsi kuwa na gharama kubwa hivyo kushindwa kumudu hivyo basi ni vyema zikaangaliwa upya.
Serikali ianzishe mikakati maalumu ya kuwaandaa vijana katika misingi ya kuyapenda masomo ya Sayansi kwa lengo la kuwa walimu watakaobobea katika ufundishaji wa masomo hayo yatakayowasaidia wanafunzi kujitegemea na siyo kutegemea ajira.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment