20 September 2012

Kuzomewa Waziri Pinda UVCCM yamvaa mbunge




Daud Magesa,Mwanza na Zourha Malisa, Dar

KITENDO cha wananchi kumzomea Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, kinaonekana kuanza kuwachang'anya viongozi wa CCM, ambapo Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), umetoa tamko likimhusisha mbunge wa Jimbo la Nyamagana kwa tiketi ya CHADEMA, Bw. Ezekiel Wenja, kuwa aliandaa mpango huo.


Kauli hiyo ilitolewa  Katibu wa UVCCM Mkoa wa Mwanza, Bw.Elias
Mpanda, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa tamko la kulaani kitendo hicho.

Alidai mbunge wa Jimbo la Nyamagana anahusika kuwanununlia viroba vya pombe vijana ili wamzomee Waziri Mkuu, Bw.Pinda kwenye
mkutano huo.

“Bw.Wenje tunaheshimu ni mbunge wetu, salamu alizokataa kuzitoa Buhongwa alipoombwa na Waziri Mkuu, aliahidi kuzitoa Sahara na kilichotokea ni kwa Waziri Pinda kuzomewa, hivyo aliwandaa vijana kwa kazi hiyo,”alisisitiza, Bw. Mpanda na kuongeza;

“Nashangaa wanasiasa kuwatumia vijana vibaya na hili ni hatari kwa maisha yetu. Waziri Mkuu anatokana na CCM, sisi UVCCM tunachukia kuona anazomewa, wakati anazumgumzia maendeleo ya nchi na mkoa wetu. Tunalaani wanasiasa waache kuwatumia vibaya vijana kujinufaisha kisiasa.”

“Anayezomea ni mlevi au kichaa siku mambo yakiharibika, waathirika wa kwanza ni kundi kubwa ni vijana kama ilivyotokea Kenya. Huwezi kusema CCM haina vijana wanachama na washabiki, inao wengi. kilichotokea uwanja wa Sahara tunakifahamu kuwa vijana wale walinunuliwa pombe na Mbunge, ” alisema

Alisema Watanzania wote ni ndugu isipokuwa wanatofauti kiitikadi. "Vijana tusifike mahali tuache kugombanishwa na wanasiasa. Ni kitendo cha aibu kiongozi kuwanunulia vijana vileo,”alisema, Bw. Mpanda.

Bw. Mpanda alisema,kujadili siasa ni kujadili maisha ya watu kwamba siasa inapoharibika shughuli za kiuchumi na maendeleo pia huharibika na kuonya vijana kuacha kuchonganishwa na wanasiasa kwa kuwa wote ni ndugu.

Alisema baadhi ya wanasiasa wanawatumia vibaya vijana ili kujinufaisha kisiasa. "Ni aibu kiongozi anayeheshimika kuwanunulia pombe vijana wafanye vurugu na kuzomea,"alisema.

Alisema kwa hali inavyojionesha hivi sasa Watanzania wanaelekea kufanana  Kenya, ambao malumbano ya mshindi wa kiti cha Urais Kati ya Rais Bw.Mwai Kibaki na Waziri Mkuu, Bw. Raila Odinga, yaliyosababisha maafa kwa watu kupoteza maisha.

Kutokana na kauli hiyo mmoja wa waandishi akata kupata uhakika wa ushahidi dhidi ya Bw. Wenje kuhusika na tukio la kuzomewa kwa Bw.Pinda, ambapo baadhi ya waandishi waliingilia kati na kuzua malumbano. AKizungumzia madai hayo, Bw. Wenje alisema ni ya kutapatapa na wanachofanya wanatafuta sehemu ya kutokea.

Alisema wakiwa Buhongwa watu wa CCM walinyimwa nafasi ya kusalimia wananchi na Waziri Mkuu, Bw. Pinda alipoona hali hiyo alimpa nafasi. "Nilisimama nikasema hii ndiyo Mwanza na salamu zaidi utazipata Sahara," alisema.

Alisema madai kuwa aliwanunulia viroba wananchi hao si ya kweli. "Watu waliojaa uwanja mzima niwanunulie viroba hizo hela nimezipata wapi...Kweli inawezeka maana uwanja mzima ulizomea," alisema Bw. Wenje na kuongeza;

"Nilikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu tangu asubuhi hadi jioni, sasa huo muda wa kuwanunulia viroba niliupata wapi?" Alisema mkuu wa wilaya alienda mbali na kusema niliwapa bangi vijana hao. "Kama wana ushahidi si wanikamate na kunipeleka mahakamani," alisema na kuongeza; "Waziri Mkuu alikiri mwenyewe kuwa ameona watu wa Mwanza."

Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kitendo cha kuzomewa  Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ni dalili za wananchi kuchoshwa na viongozi waliopo  madarakani kushindwa kutimiza ndoto zao.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw. Julias Mtatiro, alipokuwa anatoa maoni yake kuhusu tukio la wananchi mkoani Mwanza kumzomea waziri Pinda.

Alisema kuwa wananchi wamechoshwa na CCM pamoja na viongozi  waliopo madarakani, kwani wameshindwa kutimiza wajibu wao tangu walipoingia madarakani.

“Wananchi wameoneshwa kuchoshwa na chama kilichopo madarakani tangu miaka 50 ya Uhuru hadi sasa ndoto zao hazijakamilishwa ugumu wa maisha upo palepale,” alisema, Bw. Mtatiro.

Mbali na hilo, Mtatiro aliongezea kuwa kuzomewa pia kunasababishwa na kiongozi mwenye amepeleka ujumbe gani kwa wananchi wake.

“Wananchi wamefikia hatua ya kumzomea waziri mkuu kwa tabia yake ya kutotoa majibu kwa wananchi na kusababisha wananchi kukosa amani naye kama kiongozi wa ngazi ya juu” alisema.

Aliongezea kuwa kiongozi huyo amekuwa akitumiwa kwenye mfumo mzima wa utawala, hivyo hali hiyo inasababisha wananchi kuchoshwa na kiongozi huyo.

7 comments:

  1. Mtawakoma hao,wanaandaa mafia kabla ya kushika madaraka,wakishika madaraka watakuwa na vikundi vya wauwaji ili kuhakikisha utawala wao unadumu

    ReplyDelete
    Replies
    1. kweli watanzania bado hatujaelimika, hiyo kauli inaonyesha imetolewa na mtoto wa darasa la 7 ambaye ameiba mtihani

      Delete
  2. Pinda asishangae ajue watanzania wameshaamka.Hakuna kulala tena.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kabla hujasema kwa nini usitafakari kwanza? Kuna kazi kubwa sana kwa viongozi kuamsha upya moyo wa matumaini kwa Watanzania. Watanzania tumepoteza matumaini, hatuioni kesho yetu.

      Delete
  3. pinda kuzomewa ni halali kwani amepinda kisawasawa, hana maana yoyote bora ajiuzulu tu.Anazidiwa na LOWASA mara mia japo kwa kashifa za ufisadi.

    mafuteme masasi
    slp 79
    karagwe

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shame on you! kumuandika mtu hizi ni fitina tu mwanfanyia
      [mafuteme masasi
      slp 79
      karagwe]....UFE MAPEMA TENA

      Delete
  4. Waziri mkuu bwana pinda kuzomewa nidalili kuwa wananchi tumechoka na viongozi walioko madarakani kwani hawana la maana wanalofanya.

    Pinda majibu yake mengi huwa hayatoi ufumbuzi wa matatizo wananchi tuliyonayo.

    Serikali yake imeshindwa kuwalipa walimu mishahra mizuri kama watumishi wengine, walimu wamebaki kuganga njaa tu huku wakirundikiwa kazi na majukumu mazito kuliko kiasi, madaktari ni matatizo, serikali imejaa vitisho nchi nzima, viongozi wengi wa Tanzania sasa hivi wanachukia kuona watumishi wanataka kujiendeleza kielimu, huwanyima ruhusa wakidhani kuwa wakisoma zaidi watawanyanganya madaraka waliyonayo.

    Wananchi shilingi hawana wakati bei za vitu mbalimbali zimepanda hivyo wanashindwa kujikimu.

    Kwa masuala kama haya wananchi wanapoona kiongozi kama waziri mkuu wanakuwa na imani kuwa ataweza kujibu na kutatua baadhi ya kero zao jambo linalokuwa tofauti maana waziri mkuu huenda na ushabiki wa chama tu, o mara tumeweza, mara tumethubu, mara tunasonga mbele! Utasongaje mbele wakati unakotoka na ulipo huna uhakika wa kupata mlo wa mchana?

    Shame to this gov

    Romward Magugu Bakeimbweigora.
    shule ya msingi Kishanda
    wilaya mpya ya Kyerwa.

    ReplyDelete