07 September 2012

Jesus: Tunataka kuweka heshima Usiku wa Sauti na Marafiki wa kweli



Na Mwandishi Wetu

MWIMBAJI maarufu nchini ambaye anafanya kazi na bendi ya FM Academia,  Ibonga Katumbi  ‘Jesus’ amesema katika onesho la  Usiku wa Sauti wanataka kuweka heshima katika tasnia ya muziki nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Jesus alisema onesho la usiku wa sauti litaonesha kiwango chao  kipo katika nafasi gani, na pia kuonesha  mchango wao katika kukuza muziki wa Tanzania.

“Katika muziki wa vijana ukiacha kina Mzee King Kiki, Kassongo Mpinda, Msondo Ngoma na Sikinde, Diamond Sound iliweka historia na kufungua tena ushindani wa muziki kwa vijana, ramani iliyochora ndio leo inatumiwa na bendi nyingi,” alisema.

Jesus alisema ni New Silent Club wakati Diamond Sound ikiwa moja ndiyo iliweka historia ya kupandisha kiingilio, ili kupunguza idadi ya watu ukumbini lakini badala yake watu wakawa wanaongezeka kila siku.

“Baada ya sisi kutoka Diamond waliendelea lakini tukaanzisha Beta Musica nani alikuwa haimbi Bana Beta au nani alikuwa hachezi One Day Yes, leo hii watu bado wanazikumbuka nyimbo zetu… ni sawa na kina mzee Kiki, nani alikuwa anaweza kumgusa Kiki akisimama jukwaani, huyu ni mwanamuziki ambaye alikuwa na walinzi wake jukwaani, muangalie mzee Kasongo Mpinda bendi yao wao ilikuwa inapiga New Afrika wakati huo kiingilio sh 500, ili uende lazima uwe unalipwa mshahara mkubwa, wao wenyewe vaa yao tu ilikuwa hatari kabisa,” alisema.

Mwimbaji huyo ambaye anatamba na wimbo wa Fadhila kwa mama na Mugheni ambao kwa mara ya kwanza aliuimba na Diamond Sound kabla ya kuurudia Beta Musica na hivi karibuni FM Academia, alisema usiku huo unamaana kubwa sana kwao kama wanamuziki na kwa mara ya kwanza utawakutanisha pamoja baada ya miaka zaidi ya kumi na mbili.

“Wakati natoka Diamond Sound mtoto wangu wa kwanza alikuwa na miaka mitatu sasa hivi yuko sekondari, anasikia tu kazi ambazo nilifanya lakini sasa anaweza kuwaona na kuwaelewa wale ambao nilifanya kazi nao,” alisema.

Jesus katika onesho hilo atakuwa sambamba na Richard Mangustino ‘Laderacolunta ambaye alitunga wimbo wa Infarouge maarufu kama Omari mbona unajikuna, Wayne Zola Ndonga ambaye ni mtunzi wa wimbo wa Chance, Mshtahiki Meya wa Jiji, Mkuu wa Majeshi Allain Mulumba Kashama au mzee wa Kibinda Nkoi.

Katika kikosi hicho pia atakuwepo Elly Chinyama ambaye solo lake linasikika kwenye nyimbo kama Sebene, Jetou, huku rythim akisimama Adolph Mbinga ambaye alitunga wimbo wa Neema ulioipaisha Diamond kwenye chati za muziki.

No comments:

Post a Comment