11 September 2012
Elimu masafa itumike kuongeza idadi ya wataalamu nchini
Na Faida Muyomba
MFUMO wa utoaji elimu kwa njia ya masafa hivi sasa umeenea kwa nchi nyingi duniani, kutokana na kuwa na manufaa makubwa katika jamii.
Huu ni mfumo unaowawezesha wanafunzi katika fani mbalimbali, kuamua kujifunza masomo wanayoyapenda kwa lengo la kupanua weledi wao bila kuingia darasani bali kwa njia ya masafa.
Njia hii imekuwa mkombozi mkubwa katika nchi nyingi zilizoendelea duniani, kwani husaidia wanafunzi hususani wale walioko kazini kuendelea na majukumu kama kawaida tofauti na wale wanaopata masomo hayo wakiwa vyuoni.
Ni mfumo ambao ukitiliwa mkazo na serikali sio tu utasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa fani mbalimbali nchini, bali pia utasaidia kuwapatia ajira wananchi hali inayoweza kuchangia kuwepo kwa mabadiliko ya kimaendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Magalula Said, ni shahidi katika hili kwani naye anaiona elimu hiyo kuwa ni muhimu ikitumika nchini na ndio maana amesisitiza ipewe kipaumbele ili kuondoa tatizo la upungufu wa wataalamu linaloikabili nchi yetu hivi sasa.
Bw.Magalula ameyasema hayo wakati wa mahafali ya wahitimu 199 wa fani ya ukunga na uuguzi katika chuo cha uuguzi cha Geita, ambao walihitimu mafunzo hayo kwa ngazi ya cheti huku 107 kati yao wakiwa ni wale wa njia ya masafa.
"Nimefurahishwa na mfumo huu wa elimu masafa na ningelipenda kutoa wito maalumu kwa wizara ya afya na Ustawi wa Jamii kuupatia kipaumbele zaidi ili tuweze kupambana na tatizo la uhaba wa wataalamu wa afya nchini," anasema.
"Elimu kwa njia ya masafa ni utaratibu mzuri unaosaidia kupatikana wanafunzi wengi kujiunga na vyuo mbalimbali vikiwemo hivi vya mpango wa maendeleo ya afya ya msingi(MMAM) na hivyo utaleta mabadiliko makubwa ya kitaalamu hapa kwetu," anaongeza Bw. Magalula.
Anasema kuwa, mabadiliko hayo ni pamoja na kupata wataalamu waliobobea katika fani hizo lakini pia ni mfumo unaolenga kuwasaidia wanafunzi kupata fursa nyingi za kujiunga na masomo ya juu, kutokana na ukweli kuwa bila kutumia elimu masafa wanafunzi wengi watashindwa kujiunga nayo kutokana na ufinyu wa nafasi.
Anasema, serikali iko bega kwa bega kuboresha elimu kwa kutilia mkazo masomo ya sayansi kuhakikisha shule zinapata walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia, kuboresha maabara ili kurahisisha kupatikana kwa wataalamu wakiwemo madaktari, wauguzi na wakunga ili kuboresha sekta ya afya nchini.
Amewaeleza wahitimu hao kuwa, taaluma waliyoipata ni muhimu hivyo pindi wawapo katika sehemu zao za kazi wafanye kwa uadilifu wakiwatumikia wananchi kwa kuzingatia miiko na maadili ya kazi hiyo.
Amewaasa wahitimu hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na kuwa wauguzi hapa nchini wana jukumu la kuwasaidia kina mama wajawazito wakati wa kujifungua hasa katika maeneo ya vijijini.
Anatoa wito kwa watanzania wenye sifa na vigezo vya kujiunga na vyuo vya aina hiyo, wavitumie ipasavyo ili kuwapatia elimu watoto wao na kuwa huo ndio msingi bora wa maisha yao ya baadaye.
Pia anatumia fursa hiyo kuwakumbusha wahitimu hao kujiepusha na ugonjwa wa UKIMWI, ambapo amewataka kujali afya zao mahali pa kazi na mahali popote wawapo ili kuyalinda maisha yao .
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Bi.Adelina Kabakama akitoa historia fupi ya chuo anasema kilianzishwa mwaka 1977, kikiwa ni miongoni mwa vyuo 18 vilivyojengwa nchini kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania na Marekani.
Anasema, lengo la kuanzishwa vyuo hivyo ni kusaidia kufundisha wakunga wasaidizi vijijini (MCHA) kwa muda wa miaka miwili ili kuboresha afya za kina mama na watoto vijijini.
"Lakini ilipofika mwaka 1994, wizara ya afya ikaamua kubadilisha chuo toka MCHA na kuanza kutoa mafunzo ya wauguzi wa jamii daraja 'B’ (public Health Nursing School) lengo likiwa ni kuwaendeleza wakunga wasaidizi waweze kutoa huduma bora zaidi katika jamii na chuo chetu kilikuwa miongoni mwa vyuo vinane nchini kwa mfumo huu," anasema.
Anafafania kuwa, mwaka 2005 wizara ya afya ilikibadilisha na kuanza kutoa mafunzo ya wauguzi na wakunga katika ngazi ya cheti kwa muda wa miaka mitatu ambapo mwaka 2008 kulikuwa na wahitimu 37 pekee.
"Mwezi Februari mwaka 2008, wizara ilifanya mabadiliko mengine vyuo vilivyokuwa vikitoa mafunzo hayo kwa miaka mitatu sasa ikawa miwili mfumo uliolenga kupata wauguzi na wakunga wengi watakaosaidia hospitali na zahanati zilizokusudiwa kufunguliwa nchini ili wananchi wote waweze kuipata huduma hii," anasisitiza.
Anasema, hadi sasa chuo hicho kimefanikiwa kuwa na ufaulu kwa wahitimu wake kwa kiwango cha asilimia 93 na kuwa ni cha masafa na kuwa katika mahafali ya mwaka huu kulikuwa na wahitimu 107 wa kundi la kwanza.
Anaeleza kuwa, wanafunzi walioandikishwa walikuwa ni 212 lakini baadhi yao walishindwa kuendelea na masomo yao kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ada, na kuwa waliohitimu mwaka huu katika chuo hicho ni 199, wa kike wakiwa 158 na kiume 41 tu.
Ansema, mbali ya mafanikio hayo lakini pia yapo matatizo yanayokikabili chuo hicho kama vile kutokuwepo uzio, eneo la chuo kutokuwa na hati miliki, maji, uhaba wa nyumba za watumishi kwani kuna nyumba nne tu, bwalo la chakula kwa wanafunzi.
Matatizo mengine ni kutokuwa na kompyuta za kufundishia, ukumbi wa mikutano na burudani pamoja na kutokuwa na mahali pa wanafunzi kutumia kufulia na kuanikia nguo zao.
Anatoa wito kwa wahitimu kujiepusha na migomo isiyo ya lazima kazini kwa kile anachosema ina madhara makubwa kwa jamii na badala yake watumie njia mbadala itakayosaidia kupata haki yao pasipo kuathiri afya za wagonjwa.
"Napenda kuwakumbusha wahitimu wote kuwa, fani hii haifai kuleta migomo kwani njia muafaka ni kukaa meza ya mazungumzo na hakuna kitakachoshindikana katika hili, nendeni mkawahudumie wagonjwa bila kuweka mbele maslahi yenu na Mungu atawabariki kwani wagonjwa mnaowahudumia wanategemea huduma yenu kama faraja," anasema.
Hatahivyo, pamoja na nia njema ya serikali kuamua kuanzisha mfumo huo wa elimu masafa kwa wauguzi na wakunga, lakini pia ipo haja ya kuhamasisha wananchi ili wajiunge kwakua walio wengi hawajui manufaa yake.
Kama ilivyo katika sera yake ya mwaka 2007, serikali inakiri kuwa panahitajika uwepo wa wigo na ubora wa huduma za uuguzi na ukunga utakaopewa kipaumbele ili kukidhi matarajio ya wananchi.
Wizara inapaswa kuwa na mabaraza ya kitaaluma yatakayoshirikiana na Baraza la Taifa la elimu ya ufundi ili yaweze kusimamia ubora wa mafunzo yanayotolewa kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia mfumo huu wa elimu masafa kuwa endelevu na kuchangia wanafunzi wengi kuwa msaada kwao.
Si jambo la kuficha kuwa, Tanzania inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalamu wa afya katika vituo vyake mbalimbali vilivyoko vijijini, uchakavu wa majengo, upungufu wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendea kazi, hivyo pamoja na kuanzisha mfumo huu wa utoaji elimu inatakiwa pia kuyaondoa matatizo hayo ili kuleta tija kwa wananchi wake.
Elimu masafa ikitumiwa vyema, hakika itasaidia kutatua matatizo ya upungufu wa wataalam katika sekta mbalimbali nchini, hivyo upewe kipaumbele zaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment