05 September 2012

CHADEMA waibana Polisi, mauaji yatikisa


Na Waandishi Wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana kimetoa tamko la kumuomba Rais Jakaya Kikwete, awasimamishe kazi Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda.

Kimesema vigogo hao wa polisi wanapaswa kupisha uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten Daudi Mwangosi, kilichotokea Septemba 2 mwaka huu, kwenye Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Bw. John Mnyika, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mauaji yanayofanywa na polisi mara kwa mara.

Alisema Rais Kikwete anapaswa kuingilia kati suala hilo kutokana na Bw. Chagonja kutoa taarifa potofu kwa umma akidai mwandishi huyo hakuuliwa na wakati ushahidi wa picha unaonekana wazi.

“Kamanda Kamuhanda na Chagonja wanapaswa kusimamishwa kazi mara moja ili kupisha uchunguzi unaoendelea, polisi wanatoa taarifa potofu wakati picha zinaonesha wazi kabisa,” alisema Bw. Mnyika.

Aliongeza kuwa, kama Rais Kikwete atashindwa kuwachukulia hatua, itaonekana mauaji ambayo yanafanywa na jeshi hilo yanamkono wa Serikali.

Bw. Mnyika alisema chama hicho kinaitaka Serikali ifanye uchunguzi wa kina kuhusu mauaji hayo wakiamini kuwa, mauaji hayo yalikuwa yamepangwa.

Wakati huo huo, Bw. Mnyika aliwataka viongozi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali ya nchini kuwa makini kutokana na mikakati ya kupandikiza silaha ili mauaji hayo yaonekane yamefanywa na CHADEMA.

“Kuna mikakati inawekwa ili kupandikiza silaha katika maeneo ambayo CHADEMA imefanya operesheni zake na yale ambayo tumepanga kuyafikia ili chama kionekane kinahusika na mauaji,” alisema Bw. Mnyika.

Alisema katika Kijiji cha Nyororo, chama hicho kilikuwa kikifungua tawi si kufanya mkutano wa hadhara na kuhoji uhalali wa Makamu wa Rais ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, kufanya mkutano katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Bububu.

TAJONET yatoa tamko

Mtandao wa Waandishi wa Habari nchini (TAJONET), jana ulitoa tamko na kulitaka Jeshi la Polisi nchini, kuwaita waandishi wote katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaa na kuwaomba msamaha kutokana na kifo cha mwandishi mwenzao na kama litashishwa kufanya hivyo  wawaue waandishi wote.

Mwenyekiti wa Mtandao huo, Bw. William Shao, alisema jeshi hilo linaonekana kuwachoka waandishi wa habari ambapo hivi sasa limeamua kuwamaliza taratibu.


Alisema ni wakati muhafaka kwa jeshi hilo kuwaita waandishi ili kuwaomba msamaha, kuchukua hatua kwa askari aliyesababisha mauaji hayo na kama itashindikana IGP Mwema na Kamanda Kamuhanda wanapaswa kujiuzulu.

“Kama IGP Mwema, atashindwa kudhibitisha kifo cha Mwangosi, atuue waandhishi wote kwa sababu Jeshi la Polisi limetuchoka na sisi hatuna imani nalo tena,” alisema.

Alisema TAJONET, inalaani vikali kitendo cha mauaji hayo ambacho kinalenga kuua kabisa uhuru wa kupata habari kwani mwandishi huyo alikuwa kazini lakini polisi wakamuua.

“Hivi sasa kinachofanywa na polisi ni kumkamata mtu mmoja na kutangazia umma kwamba ndiye aliyemuua Mwangosi, hivyo kesi inakwenda mahakamani ili waandishi wanyamaze jambo ambalo haliwezi kukubalika, tunaamini polisi ndio wamemuua,” alisema.

PPAT wazungumza

Chama cha Wapigapicha za Habari nchini (PPAT) kimelaani mauaji ya Mwangosi wakati akitekeleza wajibu wa kazi yake.

Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mtendaji wa chama hicho Bw. Mroki Mroki, ilisema PPAT inaungana na familia yake, waandishi na Watanzania wote kulaani mauaji hayo ya kinyama.

Alisema mauaji hayo yanatishia maisha ya wapiga picha ambao huwa mstari wa mbele katika matukio mbalimbali hasa kwa kuzingatia kuwa, Jeshi la Polisi ndio chombo pekee cha usalama wa raia na mali zao lakini lilishindwa kuhakikisha Mwangosi anakuwa salama na kutekeleza wajibu wake bila matatizo.

Alitoa wito kwa IGP Mwema kuwaajibisha askari wote waliohusika na tukio hilo akiwemo Kamanda Kamuhanda ambaye anadaiwa kuchangia mauaji hayo.

“PPAT tunaungana na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Iringa (IPC), kuwazuia wanachama wetu wasiandike habari zozote za jeshi hili mkoani Iringa, tunawaomba Jukwaa la Wahariri (TEF), kusitisha uandikaji wa habarizinazolihusu Jeshi la Polisi nchini hadi watakapo wawajibisha askari waliofanya mauaji hayo,” alisema.

Waandishi Morogoro

CHAMA cha Waandishi wa Habari mkoani Morogoro (MoroPc) na Mtandano wa Habari za Kijamii nchini (MHAKITA), wameunga mkono uamuzi uliofikiwa na IPC mkoani Iringa wa kusitisha kuandika habari za jeshi hilo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Aziz Msuya, alisema MoroPc kimewataka wanahabari wote mkoani humo kuacha mara moja kuandika habari za jeshi hilo hadi watakapopewa agizo rasmi.

Alisema marehemu Mwangosi alikuwa mikononi mwa askari zaidi ya sita waliokuwa wamemzunguka hivyo hakupaswa kuuawa na askari kwani alijisalimisha mikononi mwao.

“Mwanahabari ambaye atakaidi agizo hili mkoani hapa, atetengwa na wanataaluma wote nchini, tunalaani vikali mauaji haya,” alisema.

Wakati huo huo, Rais wa MHAKITA, Bi. Merina Robart, ameunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na vyama vya waandishi wa habari nchini kutokaana na kifo cha Mwangosi.

CUF walaani mauaji

Chama cha Wananchi (CUF), kimemelaani mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi kwa Mwangosi na kusema kuwa, jeshi hilo linafanya kazi bila kuzingatia maadili.

Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema jeshi hilo linapaswa kubeba lawama kulingana na ushahidi wa kimazingira si kuisingizia CHADEMA kwa sababu liliamua kutumia nguvu kubwa na kusababisha vurugu.

“Sisi tunalaani vikali tukio hili, Jeshi la Polisi linastahili kubeba lawama kwa sababu kulikuwa hakuna sababu yoyote ya kuingilia shughuli za kisiasa za CHADEMA,” alisema.

Waandishi Ruvuma

Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Ruvuma (RPC), kimeungana na vyama vingine vya waandishi nchini kulani kitendo cha mauaji ya mwandishi mwenzao yaliyofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa.
Tamko hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Andrew Kuchonjoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Jeshi la Polisi limekuwa likionesha wazi kuwa linatumia nguvu, ubabe na matumizi mabaya ya silaha za moto ambayo hayajaweza kusaidia siku zote badala yake yanaacha maumivu na vilio kwa wananchi,” alisema Bw. Kuchonjoma.

Aliwataka viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kuendesha shughuli zao kwa kuhakikisha waandishi wa habari wanapewa ulinzi wa kutosha wanapokuwa katika mikutano yao.

CCM watoa pole

Chama Cha Mapinduizi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, kimetoa pole kwa vyama vyote vya waandishi wa habari nchini kutokana na kifo cha marehemu Mwangosi.

Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Bw. John Guninita, alitoa pole hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa chama hicho kimeguswa na msiba huo.

“CCM inatoa pole kwa wanahabari, familia yake na Watanzania kwa kumpoteza mtu muhimu katika medani ya habari, tunaiachia Serikali ifanye kazi yake pamoja na tume iliyoundwa,” alisema.

Waandishi wa habari hii ni Salim Nyomolelo, Darlin Said, Anneth Kagenda, Ramadhani Libenanga, Agnes Mwaijega, Joseph Mwambije na Heri Shaaban.

No comments:

Post a Comment