07 September 2012

Bajeti inavyokwamisha ukuaji wa elimu nchini



Daniel Samson

JUNI 1 kila mwaka Tanzania kupitia bunge hupitisha bajeti ya mapato na matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo ili kupanga utekelezaji wa miradi iliyopangwa mwaka huo.

Kwa msingi huo bajeti ndio inayotoa mstakabali halisi wa utendaji wa serikali kwa mwaka husika.

Sekta ya elimu ikiwa mojawapo inayohitaji kupewa kipaumbele kwa kuongezewa fedha ili kupunguza changamoto zinazoikabili.

Katika vipaumbele vya serikali katika bajeti ya mwaka huu mambo ya msingi yanayomgusa mwananchi wa kawaida hayajazingatiwa ambapo huduma za jamii kama elimu, afya, maji na umeme hazijapangiwa fedha za kutosha kukidhi ustawi wa jamii.

Mwananchi asipopata huduma hizo kwa ubora unaostahili hawezi kutimiza majukumu mengine ya maendeleo.

Elimu ikiwa ni huduma muhimu kwa wananchi haijapewa kipambele lakini imeingizwa katika bajeti ya rasilimali watu ambapo haijitegemei.

Nchi yoyote duniani ambayo imepiga hatua kubwa ya maendeleo imewekeza rasilimali nyingi katika sekta ya elimu ili kupata wasomi ambao watavumbua na kuleta njia mbadala za kutatua matatizo yaliyopo katika jamii.

Hali ni tofauti katika nchi yetu uwekezaji na umakini katika elimu umepungua na athari zake zinajidhihirisha hasa katika ufaulu wa wanafunzi shuleni.

Kila mwaka usajili wa wanafunzi unaongezeka huku miundombinu iliyopo kushindwa kuhimili ongezeko la wanafunzi kwa sababu ya utekelezaji mdogo wa miradi ya maendeleo.

Ongezeko la bajeti katika sekta ya elimu ni ishara kuwa shughuli za serikali zimeongezeka na hivyo matokeo chanya yanatarajiwa ikiwa tu bajeti haitaathiriwa na mfumuko wa bei na  ongezeko hilo litakidhi mahitaji ya jamii. Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 bajeti ya sekta ya elimu ilikuwa  bilioni 2,283 tofauti na mwaka 2010/2011 ilikuwa bilioni 2,045 ambapo iliongezeka kwa asilimia 12.

Bajeti inaonyesha kuongezeka kila mwaka lakini mafanikio katika sekta hii hayaridhishi kutokana na ukweli kuwa elimu ya Tanzania inashuka kila mwaka hasa katika shule za msingi na sekondari. 

Ongezeko la bajeti katika sekta ya elimu linathiriwa na sababu mbalimbali ambazo huifanya bajeti kutokidhi mahitaji ya msingi ya elimu na fedha nyingi kuishia katika matumizi ya kawaida ambayo hutengewa fungu kubwa na huku elimu yetu ikiteteleka na kukosa muelekeo wa kuinufaisha jamii.

Lakini uwiano wa bajeti ya elimu na bajeti ya taifa unapungua kila mwaka kudhihirisha kuwa serikali imepunguza mkazo wa kukuza elimu nchini. Mfano mwaka wa fedha wa 2008/2009 uwiano wa bajeti ya elimu na ile ya taifa ulifikia asilimia 20 lakini unashuka kila mwaka hadi kufikia asilimia 17 kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Uwekezaji katika sekta ya elimu bado ni mdogo ambapo fedha zinazotengwa kugharimia miradi ya maendeleo ambayo huusisha ujenzi wa mbiundombinu, vifaa vya kufundishia, nyumba za walimu, maabara na mabweni, fedha zake huwa ni chache kuliko fedha  zinazoelekezwa katika matumizi mengineyo kama  safari na posho ambapo hupangiwa fungu kubwa  zaidi.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2011/2012, ni bilioni 232.86 ambazo ni asilimia 10.2 ya bajeti nzima ya sekta ya elimu ilitengwa kutekeleza shughuli za maendeleo za sekta hii. Matumizi ya kawaida ni bilioni 2,050.14 ambayo ni sawa na asilimia 89.8 ya bajeti nzima ya sekta ya elimu.

Tofauti hii ni kubwa na inaathari katika mwenendo wa elimu, hali hii imesababisha miradi mingi iliyowekewa mipango isikamilike kwa wakati huku shule nyingi za msingi zikabiliwa na mbiundombinu isiyoridhisha na mazingira magumu kwa walimu ambao ni wadau muhimu wa kufikisha maarifa kwa wanafunzi.

Mazingira magumu ya kusomea kwa wanafunzi yamechangia kwa asilimia kubwa kushusha kiwango cha ufaulu ambapo wanafunzi wengine huitimu shule pasipokujua kusoma na kuandika.

Ikiwa bajeti nzima ya wizara ya elimu inatengewa asilimia 89.8 kwa matumizi ya kawaida ambayo huelekezwa katika kulipa mishahara, posho na kughalimia safari za watendaji katika wizara huku safari hizo zikileta matokeo hafifu katika maendeleo ya elimu nchini, ni swali ambalo linakosa majibu ya uhakika.

Bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 ni bilioni 724 imeongezeka ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana, bajeti hii ukiangalia kwa haraka haraka inaonyesha imedhamiria kuboresha elimu lakini fedha nyingi hazielekezwi katika mambo muhimu yanayoigusa sekta.

Fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo ni bilioni 92.58 ambapo bilioni zinatokana na makusanyo ya kodi za ndani lakini kiasi kilichobaki cha bilioni 74.01 kinategemea fedha za wafadhili. Bajeti hii haijalenga kuboresha elimu nchini katika kipindi cha mwaka huu kwa sababu fedha zilizotengwa katika shughuli za maendeleo ni chache na zinategemea fedha za wafadhili ambazo zinaweza zisitolewa kwa wakati kwa sababu ya mabadiliko mbalimbali.


Serikali imekuwa ikitoa matamko mbalimbali ya kupunguza bajeti ya matumizi ya kawaida ambayo ndio chanzo cha miradi mingine ya maendeleo kutokamilika kwa wakati. Tamko la serikali limebainisha wazi dhamira ya kupunguza matumizi  mengineyo katika hutuba ya bajeti ya Waziri wa fedha Juni 9, 2011 kuwa;

“Serikali itasitisha ununuzi wa samani za ofisi hususani zile zinazoagizwa nje ya nchi, kupunguza malipo ya posho mbalimbali yasiyokuwa na tija, kupunguza matumizi ya mafuta kwa magari ya serikali”.

“Kupunguza safari za ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na ukubwa wa misafara, na pia kuendelea kupunguza gharama za maonyesho na sherehe mbalimbali, na uendeshaji wa semina na warsha isipokuwa pale inapobidi na kwa kibali cha ofisi ya Waziri Mkuu”.

Pamoja na dhamira ya serikali ya kupunguza matumizi, bado suala hili limekuwa ni changamoto kubwa na hata katika bajeti za miaka miwili iliyopita hazionyeshi kupungua kwa bajeti ya matumizi ya kawaida.

Tunapozungumzia matumizi ya kawaida ni yale matumizi yasiyo ya lazima ambayo yakitengewa fedha chache hayataathiri sekta ya elimu.

Makadirio ya bajeti ni hatua ya kwanza lakini utekelezaji ni hatua muhimu sana kwa sababu fedha husambazwa katika miradi ili kuboresha elimu, lakini kumekuwa na umakini mdogo wa utekelezaji wa bajeti hasa miaka ya karibuni.

Tatizo hili ni matokeo ya mfumo mbovu wa uwajibikaji katika sekta za umma ambazo hukwamisha fedha zisifike katika maeneo yaliyokusudiwa lakini hata zikifika hazitimizi kazi iliyokusudiwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa fedha zinazopangwa katika miradi ya maendeleo hazifiki zote, mfano inaonyesha kuwa mwaka wa fedha 2008/2009 Wizara ilitumia bilioni 85.1 ilizopata toka hazina badala ya bilioni 128.5 zilizopangwa katika bajeti. Hivyo bilioni 43.4 hazikutolewa

Mwaka wa fedha 2009/2010 kiasi cha shs. bilioni 80.5 zilitolewa na hazina kati ya shs bilioni 129.3. Pia katika mwaka 2010/2011 shs. 76.8 zilitolewa na hazina kati ya shs. Bilioni 139.7  zilizopangwa. Tatizo hili linaongezeka hadi kufikia asilimia 45 kwa mwaka 2010/2011.

Ikiwa mfumo wa ukusanyaji mapato hautarekibishwa matatizo haya yataendelea na sekta ya elimu itazidi kushuka kwa sababu tu uaminifu katika utekelezaji wa bajeti umepungua au hauzingatiwi.

Elimu ni hazina muhimu kwa mstakabali wa taifa letu ikiwa matumizi ya serikali hayatazingatia mahitaji muhimu ya sekta ya elimu basi itaendelea kushuka kwa sababu hakuna mazingira mazuri ya kusomea kwa wanafunzi na walimu.

Pamoja na changamoto hizo serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha fedha za ruzuku kwa wanafunzi katika shule za  sekondari kama ilivyoainisha katika Mpango wa pili wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) ambao unatekelezwa kwa miaka mitano (2010-2014) ambapo serikali imeadhimia kutoa shilingi 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka mzima.

Swali la kujiuliza fedha hizi zinawafikia walengwa katika ngazi ya chini, umakini unahitajika zaidi kuhakikisha ruzuku hii inawanufaisha wanafunzi wote.

Serikali isitegemea fedha za wahisani katika mipango ya maendeleo kwa sababu sio fedha zote zinazoahidiwa 
zinatolewa na hivyo inaweza kuchelewesha utekelezaji miradi.

Ni vema serikali kutumia fedha za ndani kupanga bajeti ya maendeleo na bajeti ya matumizi mengineyo iwekwe katika fungu la wahisani ili kuharakisha ukuaji wa elimu nchini.

Ubora wa elimu nchini utaimarika zaidi ikiwa elimu itapewa kipaumbele katika bajeti ya nchi na uadilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo itaweka mazingira mazuri ya kusomea.

No comments:

Post a Comment