28 August 2012

Yanga yatua nchini bila Twite *Kutua leo kuikabili Mafunzo



Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga wametua nchini jana wakitokea Rwanda huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfeit akimsifia beki wake mpya, Mbuyu Twite kutokana na uwezo aliouonesha na ametamba atamuanzisha katika mechi ya kesho dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar.

Mbali na mechi hiyo, Yanga pia itacheza tena na AFC Leopards kutoka Kenya Jumamosi ikiwa ni mfululizo wa mechi za kirafiki.

Akizungumza mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana mbele ya mamia ya mashabiki wa timu hiyo, Saintfeit alisema wanawashukuru mashabiki wa Yanga waliopo jijini Kigali kwa jinsi walivyoipokea na kuipa sapoti kubwa katika mechi ilizocheza.

"Wiki moja tuliyokaa Kigali imetupa mwanga katika maandalizi yetu ya Ligi Kuu Bara, tunamshukuru mwenyeji wetu Rais Paul Kagame pamoja na Shirikisho la Soka nchini humo kwa ukarimu waliotuonesha," alisema Saintfeit.

Alisema anajivunia mafanikio aliyonayo mpaka sasa ambapo amecheza mechi 12 na kupoteza mechi moja dhidi ya Atletico ya Burundi, wakati wa michuano ya Kombe la Kagame.

Akizungumzia mechi walizocheza Kigali, alisema timu zote ni nzuri ila Polisi imezidi kutokana na jinsi ilivyokuwa ikicheza na iliwapa wakati mgumu licha ya kushinda mabao 2-1.

Alisema kutokana na maandalizi wanayofanya na mechi watakazocheza, ana imani watatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, licha ya ligi hiyo kuonekana itakuwa na ushindani.

Kocha huyo alisema kesho watacheza na Mafunzo na Jumamosi wataumana na Leopards, mechi ambazo zitampa mwanga wa kupata kikosi cha kwanza kwani hivi sasa kikosi chake kina wachezaji wengi wazuri.

Mbali na hilo, pia alizungumzia kiwango cha Twite pamoja na kwa nini hakusafiri na wenzake.

"Twite alijiunga na wenzake Jumanne usiku na katika mechi ya kwanza alicheza kipindi kimoja dhidi ya Rayon Sports, nimefanya hivyo ili aanze taratibu kuelewana na wenzake," alisema.

Alisema Twite ana kila sifa ya kuwa mchezaji kwani ana nguvu na kumiliki mpira, hivyo ataisaidia timu kwa kiasi kikubwa.

Kocha huyo alisema na katika mechi ya pili alicheza pia kipindi cha pili, ambapo alimchezesha katika nafasi ya kiungo nafasi ambayo aliimudu vizuri, hivyo ni moja ya wachezaji anaojivunia kuwa nao.

Alisema mchezaji huyo atatua nchini leo, baada ya kubaki Kigali kumalizia mambo yake ya kifamilia na katika mechi ya kesho dhidi ya Mafunzo, atamuanzisha kwa mara ya kwanza.


No comments:

Post a Comment