07 August 2012

Yanga: Hatutakaa meza moja na Simba kuhusu Yondan *Yadai kama wameona wameonewa wakate rufaa


Na Elizabeth Mayemba

KUFUATIA sakata la beki Kelvin Yondani ambaye amesajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu huu wa Ligi, klabu hiyo yenye masikani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani imesema haiko tayari kukaa meza moja na Simba, na kama wataona wameonewa wakate rufaa.


Juzi katika mkutano wa kawaida wa Simba, Mwenyekiti wa klabu hiyo alisema kwamba ametoa wiki moja mpaka ijumaa Yanga wawe wamepeleka sh.milioni 60 ili wawaachie mchezaji huyo, kinyume na hapo suala hilo litaenda mbele zaidi.

Akizungumza na gazeti hili jana, mwanachama wa Yanga Ahmed Seif maarufu kama Seif Magari ambaye alimsajili mchezaji huyo alisema hawana muda wa kupoteza wa kukaa na viongozi wa Simba kwa kuwa suala hilo lipo wazi na kama wataona wameonewa basi wakate rufaa.

"Hatuna muda wa kupoteza wa kukaa meza moja na Simba tuna mambo mengi ya kufanya kama wanashida ya fedha waseme na si kuwadanganya wanachama wao, kama wanaona wameonewa wakate rufaa popote," alisema Seif.

Alisema wana vitu vingi vya kufanya na si kuanza kuvutana na klabu yoyote, kwani walifanya usajili kwa umakini na hakuna kitakachovurugika, hivyo wanaendelea na mambo mengine ya maendeleo na si kuzozana na mtu.

Seif alisema wao si wapumbavu na kumsajili mchezaji ambaye anamkataba na klabu yake, kwani kabla ya kusajili mchezaji yeyote wanafanya uchunguzi wa kina na ndipo zoezi la usajili linafuata.

Awali baada ya Yanga kumsajili Yondan na Simba kuja juu na kuonesha mkataba mpya wa mchezaji huyo, gazeti hili liliwasiliana na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ambaye anatunza mikataba ya wachezaji Sad Kawemba ambaye alisema kuwa Yondan ni mchezaji huru hivyo anaweza kusajiliwa na timu yoyote bila ya kufanya mazungumzo na Simba.

Alisema katika faili lake hakukuwa na mkataba mpya wa Yondan kutoka Simba na klabu itakayoanza kupeleka mkataba wa mchezaji huyo ndiyo itakuwa sahihi kumtumia beki huyo.

2 comments:

  1. Rage anatakiwa atunze heshima yake na sio kuropkoka kama hajasoma. kielelezo cha mkataba ni mkataba uliosaniwa pande mbili zilizoingia mkataba na si kauli ya upande mmja kuthibitisha kuwa yeye ni mchezaji halali wa timu fulani kama Rage anavyowaongopea wapenzi wa Simba, kuwa ana mkanda wa Yondani kuthibitisha kuwa yeye ni mchezaji halali wa Simba, ktk jicho la kisheria hilo halipo.

    ReplyDelete
  2. kama rage anawadanganya wanasimba katika michezo jee wananchi waliomchagua kuwa mbunge wao watamwamini vipi?

    ReplyDelete