07 August 2012
Wapinzani wa simba watua, kucheza kesho
Na Zahoro Mlanzi
WAPINZANI wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, timu ya Nairobi City Stars ya Kenya ilitarajiwa kutua nchini jana jioni,
Timu hiyo imealikwa kuja nchini kucheza na Simba katika tamasha la Simba Day ambalo hufanyika kila mwaka na kwa mwaka huu litafanyika kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumzia maandalizi ya tamasha hilo Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kwamba wapinzani wao waliwatarajiwa kutua nchini jana jioni wakiwa na kikosi kamili.
"Tunaendelea vizuri hasa ukizingatia wiki hii tuna shughuli nyingi za kijamii mpaka kufikia Simba day, kesho (leo) tutaendelea na shughuli hizo kwa kutembelea wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala," alisema Kaburu.
Alisema siku itakayofuata ndio Simba day ambapo timu yao itacheza na Nairobi City na Agosti 9, watakwenda kutembelea Kituo cha Watoto Yatima cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasif.
Baada ya kutolewa kwa taarifa hizo, gazeti hili kupitia mtandao wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), lilibaini kuwa timu hiyo ipo katika nafasi ya 13 kati ya 16 zinazoshiriki ligi ya nchi hiyo.
Katika mechi 20 ilizocheza timu hiyo katika msimu huu, imeshinda mechi tano, ikatoa sare saba na kupoteza mechi nane ambapo kutokana na matokeo hayo imefikisha pointi 22.
Ligi hiyo inaongozwa na AFC Leopards ambayo ina pointi 40, Tusker FC na SOFAPAKA zote zina pointi 36, Ulinzi Stars na Thika United zinabanana katika nafasi ya nne na ya tano zote zikiwiana kwa pointi 33.
Pia kwa upande wa upachikaji mabao kwa timu hiyo, anayeongoza ni George Odary ambaye ana mabao mawili, Boniface Onyango, Francis Thairu, George Mwangi, Justus Basweti na Levy Mwaka wakiwa na bao moja kila mmoja.
Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Nairobi City Stars itashuka uwanjani Agosti 12 kuumana na Ulinzi Stars katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment