21 August 2012

Wajumbe, watendaji wakitumika katika usajili gharama itapungua



Na Willbroad Mathias

SUALA la Sensa na uandikishwaji wa vitambulisho vya taifa pamoja na kukusanya   maoni wakati wa kutunga Katiba ni moja ya mambo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote ulimwenguni.


Muhimu huo unatokana na kwamba bila utambulisho wa mkazi wa taifa, bila kujua idadi ya watu, na bila ya Katiba iliyotungwa na wananchi wenyewe kwa taifa lolote hakutakuwepo na maendeleo  au ustawi wa taifa.

Mbali na umuhimu huo Sensa pia inasaidia kuonesha jinsi ya kupanga mikakati ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo katika taifa husika

Kwa upande wa kitambulisho kwa mwananchi, ni muhimu kwa sababu  kinamtambulisha  mwananchi wake na kupunguza uhalifu ambao unaweza kufanywa na mtu kwa kujifanya raia wa nchi husika wakati si kweli.

Pia kuwa na kitambulisho cha taifa kwa mwananchi inasaidia kufahamu  mahali anapokaa pindi anapotafutwa  kwa mazuri au kama mwananchi amepata matatizo akiwa mbali na makazi yake na hata nje ya nchi.

Kutokana na umuhimu huo, Tanzania kwa sasa iko kwenye matayarisho ya sensa kazi ambayo itakwenda sambamba na utoaji wa vitambulisho vya uraia  katika baadhi ya mikoa ili kuhakikisha inafahamu idadi halisi ya wananchi wake na kupanga mikakati ya kuwaletea maendeleo.

Kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana Serikali  imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo.

Katika sensa ya mwaka huu Tanzania imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 140 ambazo zitatumika kufanikisha kazi nzima.

Miongoni mwa kazi ambazo zitatumika fedha hizo ni pamoja na kugharimia vifaa, malipo ya makarani,usafiri na posho mbalimbali kwa maofisa wanaosimamia kazi hiyo.

Hata hivyo pamoja na nia njema ya Serikali kutenga fungu hilo, baadhi ya wadau wa maendeleo wanasema fedha hizo zingeweza kunusurika endapo itatumika njia mbadala.

Katibu Mtendaji wa taasisi isiyo ya Serikali Kutafiti na kuchunguza Matumizi mabaya ya Fedha za Umma CRFI,Bw.Andendekisye Mwakabalula anasema Tanzania  ina utawala kutoka ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya taifa.

Anasema,utawala huo umewekwa kwa kufuata Katiba ya nchi  na kanuni zake ili kufanikisha utawala bora na ustawi wa maendeleo ya taifa  kwa ujumla.

Bw.Mwakabalule anasema mfumo huo wa kiutawala ndiyo ambao tangu itungwe Katiba umekuwa ukitumika ili kumtambua mwananchi.

"Kutoka ngazi ya kijiji kuna wajumbe wa nyumba kumi. Hawa  kazi yao kubwa ni kujua kila kaya na mkaaji wake,"anasema Mkurugenzi huyo Mtendaji.

Anasema kutokana na kazi yao wanauwezo wa kufahamu idadi ya wakazi wao endapo wangepewa jukumu la kuwasilisha idadi ya watu wanaowasimia katika maeneo husika.

"Kwa kuzingatia kazi ya wajumbe wa nyumba kumi , na kwa sababu Tanzania ya leo imegubikwa na ufisadi kazi hii wangepewa wao,"anasema Bw.Mwakabalule.

Anasema,kutokana  na mara nyingi kujitokeza vitendo vya ubadhilifu wa fedha za umma pindi zinapotengwa fedha zamaendeleo ana imani wakati wa sensa vitendo hivyo havitakuwepo kama wajumbe hao watatakiwa  kuwakilisha majina yote ya wakaaji wa kila kaya.


Bw. Mwakabalula anasema pia kwa kutumia wajumbe hao wa nyumba kumi , Serikali isingetumia pesa nyingi katika kufanikisha kazi hiyo ikilinganishwa zitakazotumika sasa.

Anasema pia wajumbe hao hata kama wangetumika wakati wa  uandikishwaji wa vitambulisho ambao tayari umeshafanyika jijini Dar es Salam na kuonekana upungufu kadha wa kadha ukiwamo wa baadhi ya wananchi kushindwa kujiandikisha katika muda uliopangwa  pasingekuwepo na uharaka wa kuweka kikomo cha uandikishwaji.

"Kwa kuwa uandikishwaji wa vitambulisho ni endelevu, wajumbe  au wenyeviti wa serikali za mitaa wangepewa jukumu la kuandikishaji wananchi,"anasema Mkurugenzi huyo mtendaji.

Anasema wasiwasi wake ni kutokana na kuwepo kwa taarifa zinazodai kuwa wale walioteuliwa katika uandikishwaji hawakukidhi mahitaji yaliyotarajiwa na hii inaweza kusababisha  kurudiwa kazi hiyo  na kutumia fedha nyingine na  pengine huenda zikawa nyingi zaidi kuliko za sasa.

Anasema,kwa jinsi anavyofahamu nchi nyingi huwa zinafanya sensa kwa ajili ya ustawi wa nchi na maendeleo katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya wananchi wake kama ilivyo Tanzania.

Katibu  huyo Mtendaji anasema,hata hivyo tofauti na ilivyo kwa nchi zilizoendelea,nchi nyingi za kiafrika ikiwamo Tanzania zimekuwa zikijikuta katika kashfa ya fedha zinazotengwa kwa shughuli za maendeleo kuangukia mikononi mwa wachache.

"Kwa jinsi ufisadi ulivyokithiri Tanzania ya sasa, pesa zilizotengwa nina wasiwasi huenda zisitumike kama ilivyopangwa,"anasema Bw. Mwakabalula.

Anasema ili kuondokana na hali hiyo, Serikali inapaswa kupanga mkakati mbadala kwa ajili ya sensa ili fedha hizo ziweze kutumika kikamilifu kama ilivyoainishwa kwenye mpango mkakati wa kazi hiyo.

Bw.Mwakabalula anasema  kwa kufanya hivyo  lengo hilo  litatimia pasipokuwepo na malalamiko yoyote kutoka kwa wale waliopewa jukumu la kuhesabu watu na vitu vilivyoainishwa kwenye mpango mkakati huo.

Anasema hata kabla ya kuanza kazi hiyo kuna malalamiko mengi kutoka kila pembe ya Tanzania kuwa kumefanyika upendeleo wa kuajiri makarani wa kufanya kazi hiyo huku manung'uniko mengine yakiwa ni ya makarani ambao wamefikia hadi hatua ya kususia mafunzo.

Anaishauri Serikali kuwa makini kusimamia kazi hiyo ili kulinusuru  taifa liisingie hasara.

No comments:

Post a Comment