24 August 2012
Umakini wa makarani wa sensa utafanikisha kazi hiyo
Na Suleiman Abeid
AGOSTI 26, 2012 ni siku muhimu nchini kwa watanzania kutokana na sensa yanye nafasi kubwa katika taifa, kwani itawezesha serikali kupanga bajeti kulingana na idadi ya watu.
Sensa imesubiriwa kwa kipindi kirefu ikiambatana na semina, mafunzo na hamasa kwa wananchi juu ya umuhimu wake kwa maendeleo ya Taifa.
Mambo mengi muhimu juu ya maandalizi ya kazi hii ikiwemo mafunzo kwa wasimamizi na makarani watakaohusika na kazi hiyo yamefanyika kwa umakini mkubwa.
Ni matumaini sasa ya watanzania wote kuona kwamba kazi hii muhimu ambayo inatazamiwa kuigharimu nchi kiasi cha shilingi bilioni 147 ambazo kama zingeekelezwa katika miradi mingine ya kimaendeleo zingefanya mambo mengi hususani katika sekta za elimu na afya.
Pamoja na kuwepo hofu ya baadhi ya watanzania wenzetu ya kutishia kutoshiriki katika zoezi hili muhimu, lakini kuna kila dalili kwamba huenda watanzania hao watabadili misimamo yao na kukubali kuhesabiwa wakati serikali na vyombo vyake vikifanyia kazi maoni na ushauri wao ili yatekelezwe katika sensa ijayo ya mwaka 2022.
Mpaka sasa umuhimu wa sensa kwa watanzania wengi umefahamika kutokana na matangazo mbalimbali yanayotolewa kupitia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara inayohutubiwa na viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali ikiwemo pia viongozi wa madhehebu ya dini.
Kutokana na hali hiyo kwa sehemu kubwa wengi wetu wameelewa kwa nini Taifa linalazimika kuendesha zoezi hilo, hivyo ili liweze kufanikiwa ni kwa jamii yenyewe kushiriki kikamilifu kutoa taarifa muhimu zinazohitajika kutolewa siku hiyo ya Agosti 26, mwaka huu.
Mbali ya umuhimu wa jamii kuonesha ushirikiano wake katika kazi hii, wanaopaswa kuhakikisha kwamba takwimu sahihi zinapatikana kama ilivyokusudiwa ni wasimamizi na makarani watakaohusika na kazi hiyo ya kuhesabu watu.
Kwa mujibu wa mafunzo yaliyotolewa kwa wasimamizi na makarani hawa, suala la ujazaji wa madodoso kwa uangalifu na umakini mkubwa ni suala muhimu sana, maana iwapo karani muhusika atazembea kwa kutozingatia maelekezo ya jinsi ya ujazaji madodoso hayo ni wazi zoezi zima litakuwa halina maana.
Kwa kawaida jabili jambo lolote liweze kukamilika kwa kiwango cha asilimia 100 ni lazima kila kitu kiwe kimetekelezwa kama ilivyopangwa, hii ina maana kwamba iwapo kuna kundi moja ambao hawatahesabiwa, ni wazi takwimu zitakazokusanywa hazitakuwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Kutofikiwa kwa lengo kunaweza kusababishwa na pande mbili, upande mmoja ni wa jamii yenyewe kutokutoa ushirikiano wao na kukubali kuhesabiwa ambapo wanaweza kufanya udanganyifu wa aina yoyote ili mradi kukwepa wasihesabiwe, hapa ni wazi takwimu hazitakuwa sahihi.
Upande wa pili ni wa makarani ambao watafanya kazi zao kinyume na mafundisho waliyofundishwa katika ujazaji wa madodoso.
Hapa ndipo katika eneo nyeti na muhimu kuliko hata la wale watakaokwepa kuhesabiwa, maana iwapo karani atavuruga madodoso yake haitokuwa rahisi kupata takwimu sahihi za eneo atakalokuwa amelifanyia kazi.
Lakini pia lipo tatizo ambalo kwa hivi sasa siyo rahisi kulipatia ufumbuzi wa haraka ambalo limelalamikiwa katika maeneo mengi nchini, ni tatizo la viongozi wa serikali za mitaa kutoshirikishwa kikamilifu katika maandalizi ya zoezi hili.
Viongozi wa serikali za mitaa ambao kwa sehemu kubwa ni wenyeviti wa serikali za mitaa, vitongoji na mitaa ni moja kati ya watu muhimu wanaotakiwa kushirikiana na makarani wa sensa kwa kuwaongoza katika maeneo yao wakati kazi hiyo itakuwa ikifanyika.
Mpaka sasa viongozi hao katika ngazi ya chini ya jamii hakuna sehemu yoyote walipoitwa na kupewa maelekezo angalau yale ya awali kwamba nini wajibu wao pale makarani wa sensa watakapokuwa katika maeneo yao.
Tulitegemea kwamba viongozi hao wa serikali za mitaa wangeweza kupata maelekezo au mafunzo mafupi juu ya maswali muhimu yaliyopo ndani ya madodoso yote matatu (dodoso fupi, dodoso refu na dodoso la jamii) yatakayotumika wakati wa kazi hiyo ya kuhesabu watu hapa nchini.
Dodoso fupi litakuwa na maswali 37 ambapo dodoso refu litakuwa na maswali 62 ambapo karibu maswali yote yaliyomo pia yapo katika dodoso refu huku maswali muhimu ikiwa ni yale yanayohusu:
Jina la mkuu wa kaya, majina ya watu wote waliolala katika kaya husika usiku wa kuamkia Agosti 26, mwaka huu na uhusiano wao na mkuu wa kaya, kiwango cha elimu na shughuli anazofanya au eneo anakofanyia kazi.
Utaratibu ulivyo ni kwamba kila mtu anapaswa kuhesabiwa katika eneo atakalolala usiku wa kuamkia Agosti 26, mwaka huu na hivyo iwapo ataondoka katika eneo hilo kabla ya makarani wa sensa hawajafika anatakiwa amuachie mkuu wa kaya husika majibu ya maswali yote yatakayoulizwa kabla hajaondoka.
Hapa lipo tatizo kidogo, baadhi ya wakuu wa kaya hawaelewi ni majibu yapi ya maswali yatakayoulizwa wanapaswa kuachiwa.
Ni wazi kwamba viongozi wa serikali za mitaa ndiyo waliopaswa kuandaliwa mapema kwa kuelezwa maswali yaliyopo katika dodoso ambayo majibu yake yanatakiwa kupatikana kutoka kwa watu watakaokuwa wamelala katika kaya zao siku hiyo.
Viongozi wa serikali za mitaa ndiyo wangekabidhiwa jukumu la kupita katika kila nyumba iliyopo katika maeneo yao ya uongozi wakiwaelimisha wakuu wa kaya kwamba majibu yatakayohitajika kutolewa kwa makarani wa sensa kutoka kwa watu watakaokuwa wamelala katika kaya zao ni yepi.
Kwa hali hiyo ni wazi pasingeweza kutokea mkwamo katika baadhi ya kaya kwa kukosekana kwa majibu ya maswali hayo yanayohitajika kupatikana, kwani kila mkuu wa kaya angembana mgeni wake kabla hajaondoka awe amempatia majibu hayo, lakini kwa ilivyo huenda likawepo tatizo kidogo hapo.
Hofu yangu ni kwamba baadhi ya wakuu wa kaya ni watu wenye umri mkubwa kiasi cha kutoweza kukumbuka mambo yote muhimu kwa urahisi, lakini pia taratibu za sensa zinaelekeza wazi kwamba mtu atahesabiwa sehemu aliyolala na siyo pale atakapokutwa na makarani wa sensa na atahesabiwa mara moja tu.
Kwa hali hii ni wazi kwamba elimu kubwa zaidi ilitakiwa kutolewa kwa wakuu wa kaya kupitia kwa viongozi wao serikali za mitaa ambao ndiyo waliokaribu zaidi tofauti na kiongozi mwingine.
Lipo wazo ambalo baadhi ya viongozi wetu wa kiserikali wamekuwa wakiamini kwamba wananchi wengi hivi sasa wanaelewa kila kitu kuhusiana na mambo yatakayohitajika siku ya kazi ya sensa hapa nchini kwa kuamini tu kwamba wanasikiliza au kusoma matangazo mbalimbali kupitia vyombo vya habari kama vile redio, magazeti na Televisheni.
Wazo hili ni potofu kwa kiasi kikubwa maana siyo kweli kwamba watanzania wote wanasikiliza au kumiliki vyombo vya habari kama vile redio au televisheni au kusoma matangazo mbalimbali yanayobandikwa katika mbao za matangazo hivyo si rahisi kwao kuyaelewa mambo ya sensa.
Mfano wa hili mpaka leo kuna baadhi ya watanzania hawaelewi UKIMWI unaambukizwaje pamoja na kwamba kumekuwepo na makongamano, semina, warsha matangazo na mabango mitaani, lakini nenda vijijini, bado kuna watu hawaelewi.
Kwa hali hii kulikuwa na kila sababu ya viongozi wa serikali za mitaa kupewa mafunzo ambayo yangewasaidia kuelewa ni mambo gani muhimu wanapaswa kuwaandaa wananchi katika maeneo yao siku hiyo ya kazi ya sensa na makazi nchini.
Pamoja na hali hiyo bado umuhimu na mafanikio ya sensa nchini kwa mwaka 2012 umo mikononi mwa wasimamizi na makarani watakaohusika na kazi hiyo ya kuhesabu watu kwa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa umakini mkubwa bila kukata tamaa na kutumia lugha laini pale watakapokuwa wakiuliza maswali.
Matumizi ya lugha zisizofaa au zenye kuashiria aina fulani ya ukali au kiamri za kijeshi aidha vitisho vya aina yoyote ile ni wazi yanaweza kusababisha karani muhusika kukosa ushirikiano wa wananchi katika eneo ambalo atakalokuwa amekabidhiwa kufanya kazi hiyo ya kuhesabu watu.
Natoa wito kwa wasimamizi na makarani walioteuliwa kufanya kazi hii muhimu kwa faida ya maendeleo ya Taifa kuhakikisha wanazingatia maelekezo waliyofundishwa na kujiepusha na sababu zinazoweza kuharibu zoezi zima ikiwemo uzembe wa kuharibu madodoso.
Serikali inapaswa kuhakikisha inatoa ushirikiano wa karibu kwa wasimamizi na makarani wote watakaohusika na kazi hii kama vile suala la posho ambalo tayari limeonesha kila dalili za kupigiwa kelele na makarani waliokuwa katika mafunzo ya siku 10.
Kwa watanzania, kushiriki Sensa ni muhimu kwa sababu kutaipa nafasi serikali kufahamu mahitaji ya wananchi wa kila rika, mahali walipo na watu wenye mahitaji maalum. Sensa kwa Maendeleo, Jiandae kuhesabiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment