24 August 2012

Uboreshaji maduka ya dawa, kuimarisha afya za wananchi.


Na Willbroad Mathias

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini(TFDA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na shirika lisilo la kiserikali la Marekani la Management Science for Health (MSH), imekuwa ikitekeleza Mpango wa Kuboresha maduka ya dawa Baridi (DLDBs) ili yawe ya dawa Muhimu (ADDO).

Mpango huu umekuwa ukitekelezwa kupitia fedha za serikali na wafadhili na hadi sasa mikoa 18 kati ya 25 nchini imefikiwa na mpango huu.


Hata hivyo, kutokana na fedha kutotolewa kwa wakati, na pengine kutotosheleza mahitaji, utekelezaji wake umekuwa ukifanyika taratibu mno.

TFDA imekuwa ikihamasisha halmashauri na manispaa pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wamiliki na watoa dawa hapa nchini,kuchangia gharama za utekelezaji wa mpango huu ili kuufanya uwe endelevu.

Utaratibu wa wamiliki na watoa dawa kuchangia gharama za mafunzo ni utekelezaji wa sera ya serikali ya kushirikisha sekta binafsi (PPP) katika utoaji huduma za jamii.

Inakadiriwa kuwa asilimia kati ya 35 na 40 ya Watanzania  zaidi ya milioni 40, wananunua dawa kutoka maduka ya dawa baridi.

Utekelezaji wa mpango wa maduka ya dawa muhimu ni matokeo ya utafiti uliofanywa na MSH kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia TFDA, ambao ulithibitisha kuwepo kwa matatizo yanayohusu uendeshaji wa maduka ya dawa baridi unaokiuka sheria kwa kiasi kikubwa na unaohatarisha afya za watumiaji.

Maduka karibu yote yamekuwa yakiuza dawa za moto kinyume cha sheria, kutokuwepo na wauzaji wenye ujuzi wa dawa, utumiaji wa majengo yasiyofaa kuuzia dawa, kutoa huduma za tiba, tohara au hata utoaji mimba.

Pamoja na hayom, kumekuwepo pia na uanzishwaji holela wa maduka ya dawa baridi katika maeneo mbalimbali ya miji na vijiji ambayo yamekuwa yakinunua dawa kutoka katika maduka ya jumla kwa kutoa taarifa za udanganyifu.

Udanganyifu huu unafanywa kwa lengo la kupata dawa za moto kinyume cha sheria, kuuza dawa zisizosajiriwa na zilizokwisha muda wa matumizi na dawa zingine zimekuwa zikiuzwa kinyume cha sheria kwani dawa zinazotolewa na serikali lazima zipitie katika vituo vya afya vya serikali tu na si vinginevyo.

Yote haya yanasababisha Sera ya Afya ya Taifa ya kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya ulio salama na unawafikia Watanzania wote isifanikiwe.

Kwa kukabiliana na hali hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia TFDA na kwa kushirikiana na MSH imebuni mpango wa maduka ya dawa muhimu uliofanyiwa majaribio Mkoa wa Ruvuma mwaka 2002-2005 kwa msaada wa taasisi ya Kimarekani ya ‘Bill and Melinda Gates Foundation’.

Mpango huu ulianzisha maduka mbadala yaani maduka ya dawa muhimu mijini na pembezoni mwa miji hapa nchini.

Nia ilikuwa kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya maeneo ya mijini na pembezoni mwa miji kwa upande wa Tanzania Bara yanatumia dawa zenye ubora na kutoa huduma kwa wahudumu wenye mafunzo na waliothibitishwa na mamlaka husika mwaka 2010.

Mpango huu ulilenga kuboresha huduma za dawa uliyohakikiwa, upatikanaji wa dawa muhimu nchini, utoaji wa huduma muhimu na kuwezesha huduma zake kuwa  nafuu na zinazopatikana kwa wateja mijini na pembeni mwa miji.

Kwa hiyo, kulikuwa na haja ya kuwataarifu wadau kuhusu mpango wa maduka muhimu, sehemu ambayo maduka hayo yatajengwa na kukaguliwa kabla ya kuwapa mafunzo watoa huduma, wamiliki na wakaguzi na hatimaye maduka muhimu ya dawa kuangaliwa na kutolewa tathmini.

Maduka muhimu ya dawa yalizinduliwa kwa mara ya kwanza nchini Mkoani Ruvuma mwezi Agosti na tathmini ya mradi wa majaribio ulionesha maboresho ya hali ya juu katika utoaji huduma bora na dawa salama.


Hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, mikoa 18 kati ya 25 ilikuwa tayari imefikiwa na mpango wa ADDO na mikoa saba mingine mpango huu ulikuwa umefikia hatua nzuri ya utekelezaji, ambapo watoa dawa wapatao 11,872 walikuwa wameshapatiwa mafunzo nchi nzima. 

Aprili  21, mwaka huu watoa dawa 1,366 kutoka manispaa ya Temeke, Ilala na Kinondoni walitunukiwa vyeti na Katibu Tawala Dar es Salaam Bi Theresia Mbando, baada ya kuhitimu mafunzo ya wiki tano ya ADDO.

Mafunzo hayo yalikuwa matokeo ya mkutano wa pamoja wa TFDA kwa kushirikiana na Baraza la Famasia manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke na wamiliki wa maduka ya dawa baridi uliofanyika Januari 17, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kama ilivyofanyika Dar es Salaam, uchangiaji wa gharama za mafunzo ya mpango wa ADDO kwa wamiliki wa maduka na watoa dawa ulifanyika pia wilaya za Kahama, Meatu, Bariadi, Tunduru, Songea Mjini na Vijijini, Namtumbo, Mbinga, Kilosa, Morogoro Mjini, Kilombero na Mbeya Mjini.

Wilaya nyingine ni Mbarali, Moshi Mjini na Vijijini, Kilindi, Dodoma Mjini, Lindi Mjini na Vijijini, Njombe, Kyela na Mkuranga.

Katika hotuba yake kwa mgeni rasmi siku ya kufunga mafunzo ya watoa dawa jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Hiiti B. Sillo, anasema: “Nafurahi kuona kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wahitimu wa mafunzo ya ADDO ni akina mama''

Anaongeza tena kuwa'' Kama mjuavyo, kumwelimisha mwanamke ni kuielimisha jamii nzima na hii imejidhihilisha leo hii ndani ya ukumbi huu.”

Naye mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk Mbando, aliwashukuru wahitimu wa mafunzo kwa ushiriki wao na wadau wengine walioshiriki kuanzisha mpango huo wa ADDO.

“Idadi hii kubwa ya wahitimu ni mafanikio makubwa. Nachukua nafasi hii kuwashukuru TFDA kwa kuanzisha programu hii muhimu,” aliongeza Dk Mbando.


Anaendelea kusema kwa'' kila mmoja wenu atekeleze kwa vitendo yale aliyojifunza kwa kutoa huduma bora na kwa kuheshimu sheria zilizopo,elimisheni jamii kuhusu programu ya ADDO na namna ya kuanzisha na kuendesha maduka ya dawa muhimu,”.

Akizungumzia juu ya programu ya mafunzo ya TFDA, mmoja wa wamiliki aliyeshiriki mafunzo hayo, Dk Moza Mandwanga, anasema “Nimejifunza mengi wakati wa mafunzo Maduka mengi ya dawa baridi hayafuati utaratibu uliowekwa na mamlaka husika''.

Anasema kwamba, Kuna vigezo vinavyotakiwa kufuatwa kama vile ukaguzi wa mahali duka lilipo, usafi wa mazingira na watoa dawa wawe wamefanya mafunzo na wana vyeti.

Anasema wamiliki wa maduka waliofanya mafunzo na wenye vyeti vilivyotolewa na TFDA tu watakaoruhusiwa kuanzisha na kuendesha maduka ya dawa muhimu nchini.

Dk Mandwanga anatoa wito kwa TFDA kuhakikisha mafunzo haya yanakuwa endelevu na yanawanufaisha Watanzania wote na kuwapa vijana fursa za ajira.

Mshiriki mwingine, Bw Amos Deogratias Makweba, mkazi wa Mtoni-Kijichi Mbagala Kuu, anasema mafunzo haya yamemsaidia sana kuongeza uelewa kuhusu ni nini anatakiwa akifanye na umuhimu wa kutunza kumbukumbu za wateja wake.

Amejifunza pia viashiria vya dawa bora, viashiria vya dawa zilizoharibika, dawa zisizo na viwango (haramu) na zile ambazo muda wake wa matumizi umepita na utaratibu wa kuziharibu zawa mbovu na pia namna ya kuanzisha maduka ya dawa muhimu.

“Viashiria vya ubora wa dawa ni pamoja na dawa iwe imesajiriwa na mamlaka husika, iwe kwenye kizungushio chake asilia, umbile lake na muda wa kuisha kutumika uwe unaonekana. Viashiria vya dawa mbovu ni pamoja na dawa kupoteza ubora wake kwa kubadilika rangi, dawa za vidonge kuyeyuka na kama ni capsules kuganda,” anasema.

Wakufunzi wa ADDO kulingana na Kanuni za TFDA za 2008 ni wauguzi wasaidizi, wauguzi-wakunga, matabibu waandamizi na wasaidizi na wafamasia wasaidizi.

Baada ya kutungwa kwa Sheria ya Famasia ya mwaka 2011,  shughuli zote za programu ya ADDO zinaratibiwa na Baraza la Famasia la Tanzania baada ya TFDA kuwa imekamilisha mpango wake nchi nzima.

Makabidhiano ya shughuli za ADDO kwa mikoa ambayo programu ya ADDO inatekelezwa yamekuwa yakifanywa na Baraza la Famasia isipokuwa  kwa mikoa sita ya Dar es Salaam, Mwanza, Kagera, Arusha, Tabora na Kilimanjaro ambako bado utaratibu huu uko katika hatua ya mwisho ya utekelezaji wake. 



No comments:

Post a Comment