16 August 2012

Simba watamba kunyakua Super 8



Na Mwali Ibrahim

UONGOZI ya Simba umetamba kufanya maajabu katika hatua ya nusu fainali ya pili ya michuano ya Super 8, ambapo leo watashuka kuumana na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia kutakuwa na mechi nyingine ya nusu fainali ya kwanza itakayopigwa saa 8 mchana katika uwanja huo kati ya Mtibwa Sugar na Jamhuri ya Pemba.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema wamejipanga kuhakikisha wanatinga fainali na kunyakua kombe hilo pamoja na sh. milioni 40 zinazowaniwa.

"Najua Azam ni timu nzuri na tumekuwa tukicheza nayo na kuvuta hisia za mashabiki wengi, lakini sisi tumejiandaa vyema hata wachezaji wetu wanawajua wapinzani wetu hivyo hakuna tatizo kwani tunaimani tutapita katika hatua hii," alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema mashindano ya mwaka huu yamekuwa na changamoto nyingi kwao na waandaajia pia, ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho kwa ajili ya michuano ya mwakani.

"Changamoto ni nyingi, lakini baada ya kumalizika mashindano haya tutakutana pamoja na wadhamini ili kufanya tathimini na kuangalia upungufu huo kwa ajili ya kuyaboresha mwakani," alisema.

Kwa upande wake kocha wa Jamhuri, Ameir Machano Chua amewataka wadhamini pamoja na TFF kuangalia upya miezi wanayopanga mashindano hayo, kwani ya mwaka huu yamewapa wakati mgumu kutokana na kuendana na mwezi wa Ramadhani, ambapo wachezaji wao wanafunga lakini ameahidi kuchukua ubingwa huo kwa mara ya kwanza.

No comments:

Post a Comment