17 August 2012
Oluoch: Nipo tayari kujiuzulu kama itabainika CHADEMA ilitupa fedha
Na Esther Macha, Tunduma
KAIMU Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Taifa, Bw. Ezekial Oluoch, amesema yupo tayari kuachia nafasi aliyonayo ndani ya chama hicho kama itathibitika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiliwapa fedha ili kutimiza azma yao ya mgomo uliositishwa na Mahakama.
Bw. Oluoch aliyasema hayo juzi baada ya kutembelea Ofisi za Mamlaka ya Mji mdogo wa Tunduma, Wilaya Mpya ya Momba, mkoani Mbeya ili kujionea uharibifu uliofanywa na wanafunzi waliofika katika ofisi hiyo kudai haki ya kufundishwa Juni 30 mwaka huu.
Alisema kuna uvumi unaodai kuwa, mgomo wa walimu ulichangiwa na CHADEMA ambacho kilitoa fedha kwa CWT ili kufanikisha azma hiyo jambo ambalo halina ukweli wowote.
Bw. Oluoch alisema kama itathibibitika mgomo huo ulitokana na ushawishi wa CHADEMA, yeye atakuwa tayari kuachia nafasi yake ndani ya CWT na kurudi kufundisha darasani.
“Ikithibitika tunapewa fedha na chama hiki cha siasa kama inavyodaiwa na Serikali ili kufanikisha zazma ya mgomo, mimi nitajiuzulu nafasi yangu na kurudi darasani kufundisha.
“Serikali inadai mimi na Rais wa CWT, Bw. Gratian Mukoba tulipewa fedha na CHADEMA, ili tuhamasishe mgomo wa walimu nchi nzima jambo ambalo halina ukweli wowote,” alisema.
Aliongeza kuwa, wanachokifanya wao ni kudai masilahi ya walimu na hawafungamani wala kushinikizwa na chama chochote kwani mgomo huo ulipigiwa kura na walimu wote na kuungwa mkono ambapo kila mwalimu alikuwa tayari kushiriki si vinginevyo.
Alisema Serikali haiwatendei haki kwa kuwahusisha viongozi wa CWT na ufadhili wa CHADEMA ili kufanikisha mgomo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment