17 August 2012

Mtoto wa miezi mitano aokotwa jirani na jalala



Na Cresensia Kapinga, Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamsaka mwanamke aliyemtupa mtoto wake wa miezi mitano akiwa mtupu katika eneo la Majengo, Manispaa ya Songea, mkoani hapa, jirani na jalala la kutupia taka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Deusdediti Nsimeki, alisema tukio hilo limetokea juzi saa moja usiku katika Mtaa wa Majengo.


“Mtoto huyu ni wa jinsia ya kiume ambapo mtu aliyemuona ni mwendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu 'yeboyebo', ambaye alisikia sauti ya mtoto akilia katika eneo la tukio,” alisema.

Alisema baada ya kusimamisha pikipiki yake na kusogea eneo hilo, alimuona mtoto huyo akiwa amelazwa chini hivyo alikwenda kwa wakazi wa eneo hilo na kuwaita ili wakashuhudie alichokiona.

“Majirani walipofika eneo hilo walimkuta mtoto akilia sana baada ya kupigwa na baridi kali hivyo walimchukua, kumpeleka Kituo cha Polisi na kupewa PF3 ili wampeleke hospitali akatibiwe,” alisema.

Aliongeza kuwa, hivi sasa mtoto analelewa na msamalia Bi. Fatuma Ndimbangi, ambaye amejitolea kumlea lakini vipimo vimeonesha mtoto huyu hajalala muda mrefu na aliishiwa nguvu,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wanachi waliohojiwa na gazeti hili walidai kusikitishwa na kitendo hicho na kuliomba Jeshi la Polisi kufanya msako mkali ili mama wa mtoto huyo aweze kukamatwa.

No comments:

Post a Comment