29 August 2012

Mrema azidi kumshtaki Kimaro


Na Gift Mongi, Moshi

MBUNGE wa Vunjo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Bw. Augustine Mrema, ameendelea kumshtaki kwa wananchi mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Bw. Aloyce Kimaro (CCM), kwa madai ya kupora ardhi zaidi ya ekari 10, zilizopo katika Mji Mdogo wa Himo wakati wa uongozi wake.

Bw. Mrema aliyasema hayo juzi katika mikutano ya hadhara iliyofanyika maeneo ya Uuwo na Lole, Kata ya Mwika Kaskazini.

Alisema Bw. Kimaro ambaye alimaliza muda wake hakuwa mchapa kazi bali ni mtafuta mali na alitumia madaraka aliyopewa na wananchi kujimilikisha ardhi katika eneo hilo.

“Hakuna uongozi wowote ulioshirikishwa katika mchakato wa kupata ardhi hii licha ya eneo hili kuwa na uhaba wa ardhi kwa shughuli za ujenzi wa shule hata hospitali.

“Yeye aliona ni sahihi wananchi kukosa fursa hii kwa kuchukua eneo lenye ekari kubwa, ni vyema akarudisha ardhi hii mikononi mwa wananchi ili waweze kuitumia kwa shughuli za maendeleo kwani hivi sasa hakuna kitu kinachofanyika,” alisema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Himo, Bw. Jamal Husein, alikiri kuutambua mgogoro huo na kudai Bw. Kimaro hajawahi kupita ofisi za kijiji kuomba ardhi hiyo bali alitumia njia za panya kuipata.


Kwa upande wake, Bw. Kimaro alisema ardhi hiyo aliipata kihalali na nyaraka zote anazo hivyo siasa haziwezi kubadilisha umiliki wa ardhi hiyo isipokuwa Rais ndiye mwenye uwezo huo.




No comments:

Post a Comment