29 August 2012

Jengo la Utawala Mombo laungua



Na Yusuph Mussa, Korogwe

JENGO la Utawala la Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, juzi usiku limeteketea kwa moto pamoja na nyaraka zote za Idara ya Fedha, Masjala, Ofisi ya Mtendaji wa Mamlaka hiyo na Mwenyekiti wake.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo, alifika eneo la tukio jana saa mbili asubuhi akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na kukuta kila kitu kimeteketea.

Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo, Bw. Richard Rwizile, alisema ni mapema kusema chanzo cha moto huo, lakini kutokana na mgogoro uliopo kati ya mamlaka ya mji huo na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ni muhimu ikaundwa tume kuchunguza.

Mmoja wa walinzi wa jengo hilo, Bw. Yohana Msiki, alisema walisikia kitu kinalia katika eneo la tukio na kuona moto ukiwaka kwa kasi ya ajabu lakini gari la zimamoto lilifika eneo hilo asubuhi likitokea mjini Korogwe umbali wa kilomita 43.

Kwa upande wake, Bw. Gambo alisema hataacha jambo hilo lipite hivi hivi hivyo lazima aunde tume ambayo itabeba wajumbe kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Shirika la Umeme nchini (TANESCO), polisi na wadau wengine ili kujua chanzo cha moto huo.

Hata hivyo, mkazi wa mji huo, Bw. Miraji Mkongo, alisema wana mashaka na ajali hiyo wakiamini ni hujuma kwani wamekuwa wakililia mji huo kuwa halmashauri kwa zaidi ya miaka nane.




No comments:

Post a Comment