21 August 2012

Milovan: 'First Eleven' nitaipata Agosti 25



Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, itamsaidia kupata kikosi cha kwanza kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba imeweka kambi jijini Arusha kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii inayotarajiwa kuchezwa Agosti 25, mwaka huu pamoja na Ligi Kuu.


Akizungumza kwa simu akiwa Arusha jana, Milovan alisema kwa kuwa kikosi chake kina wachezaji wengi wapya, anatarajia kupata kikosi cha kwanza katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii.

"Kikosi changu ni kizuri kila mchezaji anajituma kadri ya uwezo wake, lakini pia mechi yetu na Azam FC itanisaidia kupata kikosi cha kwanza na kuangalia upungufu katika kikosi changu," alisema Milovan.

Alisema wachezaji wake wapya wanaonesha uwezo mkubwa katika mazoezi, lakini kipimo kizuri pia ni katika mechi ambayo anaimani itakuwa na presha kubwa kwa kila mmoja kutaka kutwaa Ngao ya Jamii.

Pia kocha huyo alisema katika kikosi chake, hataacha kuwatumia baadhi ya wachezaji wa kikosi cha pili wenye umri chini ya miaka 20, kwani wengi wao walipata uzoefu zaidi katika msimu uliopita wa ligi.

Aliipongeza timu B ya Simba kwa kutwaa kombe la Super 8 na kuwataka waongeze bidii zaidi, kwani watakuja kuwa msaada mkubwa katika timu hiyo baadaye.

No comments:

Post a Comment