16 August 2012
Mexime azishangaa Simba, Yanga
Na Mwali Ibrahim
KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar Meck Mexime, amezishangaa klabu zinazogombania wachezaji wa nje ya nchi na kuwasaini kwa fedha nyingi huku wakiwaacha wachezaji wa hapa nchini wenye uwezo mkubwa.
Timu zinazoonekana kugombea wachezaji ni Simba na Yanga, ambazo zipo katika mvutano wa mchezaji Mbuyu Twite wa timu ya APR ya Rwanda pamoja na Kelvin Yondan aliyekuwa akikipiga Simba msimu uliopita.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mexime alisema kuwagombania wachezaji wa nje ni kuwapa kichwa ambapo baada ya kuwasajili wanawafukuza kwa muda mfupi kutokana na kuonesha uwezo mdogo, huku wakiwa tayari wameshawapa mamilioni ya fedha.
"Hapa nchini tuna wachezaji wazuri na wenya uwezo mkubwa wa kucheza soka, lakini nashangaa klabu nyingine zinawapa nafasi ya juu wachezaji wengine na hata kulumbana kwa ajili yao, kitu ambacho si sahihi na kinanyima fursa wachezaji wetu katika kuendelea vipaji vyao," alisema.
Aliongeza kuwa wapo wachezaji wazuri kama Said Bahanuzi, ambaye aliibuka mfungaji bora katika michuano ya Kagame ambaye angefaa kuwaniwa na timu katika usajili, lakini wapo radhi kumwaga fedha kwa wachezaji wa nje na kuwatumia kwa muda mfupi.
Alisema hali hiyo inawafanya wachezaji wa nje kuona kama klabu za Tanzania ni za kuchukua fedha na kutangazwa kwa muda na baadaye kutimuliwa lakini akiwa amenufaika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment