16 August 2012

Mawakala wa sensa Geita wasusia mafunzo


Na Faida Muyomba

ZAIDI ya makarani 150 waliokuwa wakihudhuria mafunzo ya Sensa ya Watu na Makazi, katika Wilaya ya Geita, mkoani Mara, jana wamegoma kuendelea na mafunzo wakidai kutolipwa fedha zao.

Mgomo huo ulianza asubuhi kwenye kituo cha mafunzo kilichopo katika Shule ya Sekondari Katoro, ambapo mafunzo hayo yalikuwa yakishirikisha makarani kutoka tarafa ya Busanda na Buntundwe.


Wakizungumza na Majira, makarani hao walisema hawako tayari kuendelea na mafunzo bila kulipwa stahiki zao na kuwa omba omba kwa sababu ya kukosa fedha za kununulia chakula na kulipia gesti walizofikia kwani tangu waanze mafunzo hayo hawajalipwa.

“Tumeamua kususia mafunzo haya na kutoka ndani ya chumba cha mafunzo, walinzi waliokuwa eneo hili walitukagua ili kuhakikisha hatuondoki na mabegi yenye nyaraka tulizokuwa tukizitumia mafunzoni,” walisema makarani hao.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Omary Mangochie, alikiri makarani hao kususia mafunzo baada ya kutolipwa stahiki zao hadi jana.

“Kimsingi tatizo haliko kwetu bali limetokana na matatizo ya kibenki ambayo yako nje ya uwezo wetu, nilikuwa na makarani hawa siku ya Jumapili nikawaeleza hali halisi kuwa kuna tatizo la uhamishaji fedha kutoka Benki ya NBC na NMB,” alisema.

Alidai kushangazwa na hatua ya makarani hao kususia mafunzo kwani uhakika wa fedha hizo kuzipata jana ni mkubwa ili waweze kulipwa stahiki zao hivyo hawakustahili kugoma.

No comments:

Post a Comment