31 August 2012

Mahakama yawaachia wanafunzi 51 UDSM


Na Grace Ndossa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana imewaachia huru na kuwafutia mashtaka wanafunzi 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya kufanya mikusanyiko na maandamano bila kibali.


Uamuzi huo ulifikiwa mahakamani hapo jana baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kufika makahamani ili kutoa ushahidi ambapo Hakimu Waliarwande Lema, alidai kesi hiyo imeshaairishwa mara mbili kutokana na upande wa mashtaka kutofika mahakamani.

Alidai mara ya kwanza kesi hiyo iliahirishwa Julai 12 mwaka huu kutokana na ombi la upande wa mashtaka na kudai askari ambao walitakiwa kutoa ushahidi mahakamani walikuwa katika mgomo wa madkatari ambapo mahakama ilikubaliana na ombi hilo.

Hakimu Lema alidai, kutokana na ahirisho hilo, kesi hiyo ilipangwa tena Agosti 13 mwaka huu na upande wa mashtaka uliomba ahirisho lingine wakidai askari hao wapo katika mchakato wa sensa.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Lema alitupilia mbali sababu hizo na kudai kama kesi hiyo itapangwa tena, upande wa mashtaka utakuja na sababu nyingine.

Washtakiwa hao waliachiwa huru kutokana na kanuni ya kuendesha makosa ya jinai  225, kifungu cha tano sura ya 20 na kuwafutia kesi.

Novemba 14 mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza ambapo wakili wa Serikali Bw. Ladslaus Komanya, alidai katika eneo la Mlimani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Shtaka la pili ni washtakiwa hao wakiwa katika mkusanyiko haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi la Polisi waliwataka watawanyike lakini walikahidi amri hiyo.

No comments:

Post a Comment