02 August 2012
CWT sasa wajivunia mafanikio ya mgomo
Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimejivunia mafanikio ya mgomo waliouitisha wakidai umefanikiwa kwa asilimia 95.7 na kutangaza mpango wa kuzidisha mapambano hadi kieleweke.
Pia chama hicho kimeitaka Serikali kuacha vitisho kwa walimu ambao wameunga mkono mgomo huo na kudai kuwa, vitisho hivyo havitasaidia kupatikana muafaka.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho, Bw. Gratian Mukoba, alisema kila siku walimu wazidi kuunga mkono mgomo huo kwa kuwa ni halali na hawahitaji kumsikiliza mtu mwingine zaidi ya CWT.
Alisema mgomo ulipoanza Jumatatu wiki hii, uliungwa na walimu kwa asilimia 90, lakini siku zinavyozidi kwenda idadi inaongezeka na kuwataka walimu waendelee kushirikiana ili wapate haki zao ili waweze kutoa elimu bora si bora elimu.
“Walimu wanatakiwa kushiriki mgomo kikamilifu kwani upo kihalali kwa mujibu wa katiba ya nchi na ile ya chama chetu, kimsingi walimu wasioshiriki mgomo huu ni wanafiki na wanajipendekeza ili wapate vyeo vya upendeleo,” alisema.
Alidai kushangazwa na hatua ya Serikali na Bunge kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kutangazia umma kuwa mgomo wa walimu ni batili, huku Bunge kupitia Naibu Spika, Bw. Job Ndugai, akidai Mahakama ingetoa hukumu Julai 31 mwaka huu, saa saba mchana, wakati pande zote mbili zilikuwa hazijasikilizwa.
Alisema CWT imepokea taarifa ya kukamatwa kwa baadhi ya walimu katika Wilaya za Tarime, Rungwe, Kyela, Babati, Pwani, Morogoro na Ruvuma.
Bw. Mukoba alisema maeneo mengine watendaji wa CWT wanatishwa na wakuu wa mikoa pamoja na Kamati za Ulinzi za Mikoa ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Mecky Sadick amewatishia wanachama na viongozi wa chama na kuamuru wakamatwe, sisi tunasema mwajiri wetu si Mkuu wa Mkoa wala Wilaya, tunazidisha mapambano yetu hadi kieleweke,” alisema Bw. Mkoba.
Aliongeza kuwa, kuna uvumi unaodai kuwa wanafunzi wanaofanya maandamano wamefundishwa na walimu jambo ambalo si kweli na kuitaka Serikali kukaa mezani na CWT kwani viongozi wake wapo tayari ili kutafuta muafaka wa mgogoro huo.
Wilaya ya Kyera
Kutoka Kyera, mkoani Mbeya, Mwandishi Wetu ameripoti kuwa, Katibu wa CWT wilayani humo, Bw. Pastori Mangula, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya kwa kosa la kushawishi walimu kuingia kwenye mgomo ambao umeanza juzi.
Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Joseph Luambano, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bw. Nicholaus Charles, alisema mshtakiwa anakabiliwa kosa la kushawishi walimu wa shule tatu za msingi mjini Kyela kuingia kwenye mgomo lakini alipewa dhamana ambapo kesi hiyo itatajwa tena Agosti 28 mwaka huu.
Dar es Salaam
Uchunguzi uliofanywa na Majira jana, ulibaini baadhi ya madarasa katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam, yalifunguliwa lakini hakukuwa na wanafunzi shuleni wengi wao wakiwa mitaani.
Hali hiyo ilijitokeza katika Shule za Msingi Kijichi, Bwawani, Mbagala Kuu, na Maendeleo zilizopo Kata ya Kijichi na Mbagala Kuu, wilayani Temeke.
Katika shule zingine kama Lumumba iliyopo katikati ya jiji, walimu walionekana madarasani wakiwa wamekaa na wengine walikuwa ofisini na ubao wa ofisi uliandikwa maneno yaliyowataka walimu kudumisha mshikamano.
Maandishi hayo yalisomeka “Solidarity Forever, Solidarity for Changes, No Returning Back”, huku ofisi ya Mwalimu Mkuu ikiwa imefungwa lakini walimu hao walikataa kuzungumza na waandishi.
Mkoa wa Singida
Mkoani Singida, wazazi na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wametoa wito kwa walimu kuacha kuendelea na mgomo ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Ushauri huo ulitolewa jana wakati wazazi hao wakizungumzia athari za mgomo huo ambapo katika baadhi ya shule mkoani humo, baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba walionekana wakifundishana wenyewe bila msaada wa mwalimu.
Mwenyekiti wa CWT Mkoa humo, Bw. Darran Jumbe, alisema CWT kimetoa maelekezo kwa walimu wote waendele na mgomo hadi Serikali itakapowatimizia madai yao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bi. Salome Singano, alisema walimu 573 ndio wameunga mkono mgomo huo na wengine 67 wanaendelea na kazi.
Wilaya ya Hai
Katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, imeripotiwa walimu wameanza kupata vitisho baada ya kuanza kupita Waratibu wa Elimu Kata na Wilaya na kushinikizwa wajaze fomu zenye vipengele vitatu kikiwemo cha kukubali au kukana kushiriki mgomo.
Walimu waliozungumza na Majira kwa sharti la kutotajwa majina yao, walidai kinachofanyika sasa ni kupewa vitisho.
Habari hii imeandikwa na Rehema Maigala, Israel Mwaisaka, David John, Salim Nyomolelo na Damiano Mkumbo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WAALIMU MUSLAZIMISHE SERIKALI KUPRINT NOTI WALA GHARAMA ZA MAISHA HAYATASHUKA YOTE HAYA NI KUTOKANA NA SERIKALI KUTOKUWA NA SERA YA ELIMU MUNAFUNDISHA WANAFUNZI ILI WAAJIRIWE NA WALA SIO KUJIAJIRI MWALIMU LIMA,FUGA UWE MJASIRIAMAJI ACHA KULAZIMISHA SERIKALI IPRINT HELA KAMA BIDHAA NA CHAKULA HAKUNA HATA HELA ZINGEKUWANYINGI KIASI GANI NI SIFURI MFANO HAI DEBE LA MAHINDI NI TSHS.12000 JE UNGEKUWA NA MAGUNIA MIA MBILI UNGEKUWA NA FEDHA KIASI GANI SOMENI ELIMU YA KUJITEGEMEA YA HAYATI MWL JK NYERERE
ReplyDeletewaalimu tuwe na ushirikiano zaidi katika kupigania haki zetu kwa sababu serikali yetu imetusahau kabisa hali yetu ya maisha ni mbaya sana. kila duka tunadaiwa. jamani sisi waalimu wa Tanzania tumealaniwa nini. waalimu wenzangu tujiendeleze kielimu, tufungue miradi ili tuweze kujikomboa kiuchumi. kila mwalimu ajitaidi kijikomboa kwa sababu serikali ya ccm hajali mwalimu hata kidogo.
ReplyDeleteHONGERA SANA MAKAMANDA WA CWT