21 August 2012

ASUTA, RFE wabadilisha maisha ya wanawake Bagamoyo


Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

SERA ya Maendeleo ya Wanawake katika Maendeleo ilipitishwa na kuanza kutekelezwa mwaka 1992.

Utekelezaji wa sera hiyo umesaidia kuwepo kwa ufahamu zaidi kuhusu haki za wanawake katika ngazi mbalimbali za kufanya maamuzi na mipango.

Pia, uanzishwaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayolenga kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika nyanja mbalimbali, kutambulika kwa michango ya wanawake katika maendeleo yote ya nchi na kupewa fursa zaidi katika nyanja za siasa, uongozi, na kujiletea maendeleo ya kiuchumi.

Serikali, na mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakitoa elimu kwa wanawake kutambua haki zao za msingi ili kupunguza unyanyasaji wa kijinsia.

Kutokana na ugumu wa maisha wanawake wengi hutafuta kipato kwa kuuza miili yao bila kujali kuwa wanahatarisha afya zao.

Elimu ya kuwakomboa wanawake hao kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali na wanaharakati yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza biashara hiyo.

Bi.Farida Ally (33), mkazi wa kitogoji cha Dunda, wilaya ya Bagamoyo anasema “ Nimekuwa nikifanya biashara ya ngono kwa muda mrefu, ili kukizi mahitaji yangu ya kila siku na familia”.

“Katika biashara hii nimekumbana na mambo mengi, hata hivyo kwa sasa naona matumaini mapya katika maisha baada ya kutembelewa na Asasi ya Uwezeshaji Rika Tanzania ‘ASUTA’ ambayo ipo hapa Bagamoyo”

Bi.Ally ni miongoni mwa wakazi wa Bagamoyo ambao wamepitia katika maisha ya kuishi katika maazingira hatarishi katika maambukizi ya UKIMWI hususan kwa wanaojihusisha na biashara ya ngono.

Anasema amekuwa akijihusisha na biashara kuuza mwili wake kwa kipindi cha miaka mitatu, kazi  aliyoianza baada ya kufiwa na mumewe, hivyo kushindwa kuendesha maisha kwa kuwa alikuwa hana kazi wala mtaji wa kumuwezesha kufanya japo biashara.

Baada ya kuwa katika biashara hiyo kwa takribani miaka mitatu, akihangaika kuuza mwili wake ili kuendesha maisha, sasa ni miongoni mwa wakazi 450 wa wilaya ya Bagamoyo ambao wamepata ushauri na elimu rika jinsi ya kuepukana nayo.

Kupitia ASUTA ambayo ni Asasi ya uwezeshaji rika Tanzania, inayo fadhiliwa na Mpango wa kudhibiti maambukizi VVU Tanzania (RFE), ikishirikiana na Tume ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na Tume ya Zanzibar ‘ZAC, kumekuwepo na mwanga kwa baadhi ya vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa maambukizi ya Ukimwi baada ya kuelimishwa.

Jamii kubwa ya wakazi wa Bagamoyo mbali ya ugumu wa maisha, wamekuwa gizani kwa kuendekeza mila potofu ambayo imetanda katika wilaya humo.

“Huku hali ni tofauti na sehemu nyingine kwani wakazi wengi bado hawajazinduka na kuachana na mila potofu ambazo ni miongoni mwa vyanzo vya kuenea kwa kasi kwa maambukizi ya ukimwi katika wilaya ya Bagamoyo” anasema.

Anasema, katika biashara ya ngono aliyokuwa akifanya ilikuwa haina bei maalum ili mradi ahakikishe kuwa nyumbani anarudi na chochote hivyo suala la kufanya ngono salama huwa ni ngumu kutokana na baadhi ya wateja hukataa kutumia kinga.

Anasema wateja wengi ni madreva wa masafa marefu, watu ambao hukaa kwa muda mrefu mbali na familia zao, wanaume wenye tamaa ya wanawake na watalii .

Hali ngumu ya kimaisha inayoikabili jamii kubwa ya watanzania kimeelezwa kuwa ndicho chanzo cha baadhi ya wanawake kujihusisha na biashara ya kuuza miili yao.

Kama ilivyo katika mikoa mingine ya Tanzania kwa vijana kuwa na hali ngumu kiuchumi kutokana na vijana kukosa ajira Bagamoyo imekuwa miongoni mwa wazalishaji wa wasichana wanao jihusisha na biashara ya ngono na utumiaji wa madawa ya kulevya, uvutaji wa bangi na ngono za jinsia moja hususani kwa wanaume.

Utafiti uliofanywa  hivi karibuni umebaini kuwepo kwa hali hiyo, kumechangiwa na hali ngumu ya kimaisha ambapo vijana wengi ambao hawana ajira hushindwa kujipatia mahitaji yao ya kila siku, na baadhi huathiriwa na mila potofu zisizo na dira ya kimaendeleo.

Takwimu za Afya kwa wilaya ya Bagamoyo zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2009/2010 maambukizi ya UKIMWI kwa Bagamoyo yalikuwa 9.4 asilimia huku 2010/2011 maambukizi yalifikia 11 asilimia.

Meneja mradi wa ASUTA Bw.Prince Pastory  anasema, “Wasichana 50 wanaouza miili yao wameweza kufikiwa na waelimisha rika wetu, na kujifunza kutumia njia salama pamoja na kutafuta njia mbadala za kujipatia kipato”.

Asasi ya ASUTA ambayo imepata ufadhili wa mwaka mmoja kutoka RFE, imeweza kuzifikia kata 16 katika Wilaya ya Bagamoyo, na kuwafikia watu 450, lengo likiwa kuwafikia watu 250 kwa kipindi cha robo mwaka.

Kati yao wasichana wanaofanya biashara ya kuuza baa 70, wamepata elimu ya kujiginga na maambukizi ya UKIMWI kundi lililo katika hatari ya kupotea kutokana na kufanya ngono haramu.

Meneja mradi anasema, kundi la wauza baa wamekuwa katika mazingira hatarishi kutokana na kupata kipato kidogo, katika kazi yao ambapo kwa Bagamoyo utafiti unaonyesha kuwa wahudumu hao hulipwa kati ya Sh 35,000 hadi 45,000 kwa mwezi kiasi ambacho hakikizi matumizi muhimu.

Anasema ASUTA, imeweza kubaini uwepo wa baadhi ya familia kushawishi mabinti zao kujihusisha na biashara ya ngono, ili kuweza kukidhi mahitaji ya familia ya kila siku.

Meneja huyo anasema shughuli za kila siku za uvuvi zinazofanyika katika mto Wami na Ruvu, zimekuwa zikukufanya makundi mbalimbali ambayo huwa katika mazingira hatarishi katika kuenea kwa maambukizi ya ukimwi.

Mwelimisha Rika wa ASUTA, Nezia Manyama anasema, wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kuvifikia baadhi ya vijiji kutokana na ukosefu wa usafiri hususan kwa vijiji vilivyo pembezoni mwa wilaya ya Bagamoyo ikiwa ni pamoja na kutopata fedha za kujikimu.






1 comment: