30 July 2012
Yanga kutwaa taji la tano, Azam la kwanza *Bahanuzi, Bocco, Kiiza mvutano
Na Zahoro Mlanzi
KATIKA siku ambazo mashabiki na wadau wa soka hawatotulia sehemu moja wakisubiri muda ufike basi ni leo, ambapo mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, timu ya Yanga itaumana na Azam FC katika fainali ya aina yake itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ni fainali ya aina yake kutokana na timu zilizotinga hatua hiyo kuwa na historia tofauti ya michuano hiyo, wakati Yanga ikisaka taji la tano, Azam yenyewe inataka iweke historia kwa kushiriki mara ya kwanza na kutwaa ubingwa huo.
Michuano hiyo inafikia tamati leo baada ya mshikemshike wa wiki mbili iliyoikutanisha miamba 11 kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Yanga ambayo kwa sasa inanolewa na Mbelgiji, Tom Saintfeit ilikuwa kundi moja na timu za APR ya Rwanda, Atletico ya Burundi na El Salaam Wau ya Sudan Kusini, ilivuka hatua ya makundi kwa kuwa na pointi sita nyuma ya Atletico ambayo iliiongoza kundi hilo.
Robo fainali Yanga ilicheza na Mafunzo ya Zanzibar ambapo iliibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti 5-3 ambapo ilikutana na APR nusu fainali na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Azam yenyewe ilikuwa kundi moja na timu za Mafunzo na Tusker ya Kenya ambapo katika kundi hilo ilipita yenyewe pamoja na Mafunzo.
Robo fainali iliumana na mabingwa wa kihistoria, Simba ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na nusu fainali iliumana na AS Vita na ikaiubuka na ushindi wa mabao 2-1.
Azam ndio timu pekee ambayo kwa hivi sasa inaonekana kuzipa presha Simba na Yanga kutokana na mfumo wake wa kuendesha soka lao, hivyo itakuwa na kazi moja kuhakikisha inaweka historia.
Ikumbukwe mwaka jana, Yanga iliifunga Simba katika fainali bao 1-0 na kutwaa taji la nne la michuano hiyo, baada ya awali kutwaa kombe hilo 1975, 1993 na 1999.
Ubingwa huo wa mwaka, iliupata chini ya Kocha, Sam Timbe aliyejiunga nayo katikati ya msimu wa mwaka jana na kuiwezesha kutwaa ubingwa lakini baadaye aliondolewa.
Simba ilitwaa ubingwa huo katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002 huku timu za Kenya za AFC Leopard, Gor Mahia na Tusker zikitwaa ubingwa huo mara tano kila moja kwa nyakati tofauti.
Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, itatanguliwa na mtanange wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya APR na timu mwalikwa ya AS Vita katika mechi itakayokuwa na ushindani wa aina yake.
Makocha wanazungumziaje mechi hiyo Saintfeit wa Yanga alisema anashukuru kuifikisha timu hiyo fainali ya michuano hiyo na kazi iliyobaki ni kutwaa ubingwa.
Kocha wa Azam, Hall Stewart naye alisema ni hatua kubwa wamepiga kwa kipindi kifupi kwani kufika fainali ya michuano hiyo sio kazi ndogo.
Alisema kutinga hatua hiyo ni mwendelezo wa mafanikio ya timu hiyo baada kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho, sasa wamedhamilia kutwaa kombe hilo.
Bahanuzi vs Bocco
Ukiachana na vita ya kuweka historia kwa timu hizo lakini vita nyingine ipo kwa washambuliaji Said Bahanuzi na Hamis Kiiza wa Yanga na John Bocco wa Azam ambapo kila mmoja amepachika mabao matano katika michuano hiyo.
Wachezaji hao wanashika nafasi ya pili nyuma ya mshambuliaji wa AS Vita, Taddy Etikiama ambaye amezifumania nyavu mara sita na watakuwa wakimuombea mabaya asifunge katika mechi ya mshindi wa tatu ili wao wakifunga waweke heshima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment