19 July 2012

Wanaokipaka matope CCM kukiona-Nape



Na David John

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, ametoa onyo kwa watu wanaokipaka matope chama hicho ili kukichafua.

Alisema kuanzia sasa, CCM haitakuwa tayari kuvumilia hali hiyo badala yake itawachukulia watu hao hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Nnauye alisema wapo baadhi ya watu wanaozusha kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Wilson Mukama anataka kujiuzulu kwa sababu ya kushindwa kuelewana na sekretarieti ya chama hicho kitu ambacho hakina ukweli wowote.

“Kuna watu wanaeneza propaganda za uongo kuwa Makao Makuu ya CCM, kuna msuguano kitu ambacho hakina ukweli wowote, nitachukua hatua kwa wahusika pamoja na kuwaanika hadhalani.

“Wapo wanaosema kuna mabilioni yametolewa na  Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya ziara zinazofanywa na viongozi wa CCM na ndio chachu ya msuguano,” alisema.

Bw. Nnauye aliongeza kuwa, sio kweli kwamba Rais Kikwete ametoa fedha ili kufanikisha ziara za viongozi ambapo watu wanaoeneza uvumi huo ni waongo.

Alisema Bw. Mukama kupitia sekretarieti yake, wanafanya kazi kwa ushirikiano hata kibari cha kufanya ziara hizo kimetoka kwake hivyo wanachama wa CCM wasikubali kuyumbishwa na propaganda.

Katika hatua nyingine, Bw. Nnauye alisema chama hicho kinaendelea na ziara ya kuimarisha chama na kuangalia utekelezaji wa ilani yao katika mikoa mbalimbali nchini.

“Baada ya kumaliza ziara katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Singida na Mpanda, sasa tunakwenda mkoani Kigoma na tutafanya mkutano mkubwa ambao utahudhuriwa na Mawaziri mbalimbali,” alisema Bw. Nnauye.

Aliongeza kuwa, Mkoa huo unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya usafiri wa reli kutokuwa wa uhakika, maji na elimu hivyo Mawaziri wote wahusika watakuwepo.

Bw. Nnauye pia alizungumzi chaguzi mbalimbali za matawi na mashina ngazi ya Wilaya zinazoendelea nchini nzima na kudai kuwa, zimeonesha mafanikio makubwa.

1 comment:

  1. WAFUNDISHENI WABUNGE WENU KUWA KATIKA UWAJIBIKAJI WA PAMOJA WANATAKIWA KUUNGA MKONO BUDGET YAO WANACHOTAKIWA NI KUIBORESHA HAYA HUFANYIKA KATIKA MISING YA "PARTY CAUCAS" KINACHOSHANGAZA NI WABUNGE WA CHAMA TAWALA KUSAIDIANA NA WALE WA UPINZANI KUIKOSOA BUDGET KUICHANA HADHARANI SIJUI NI MAMLUKI WA UPINZANI HIVI HII DEMOKRASIA YA VYAMA VINGI INAELEWEKA VIZURI HIVI NANI KATIBUMWENEZI WA CHAMA BUNGENI????

    ReplyDelete