05 July 2012

Uwekezaji elimu ya ufundi utachochea maendeleo nchini



ELIMU ni uti wa mgongo katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia ambapo nchi mbalimbali duniani, zimewekeza katika sekta hiyo ili jamii kubwa isome na kutumia elimu waliyonayo  kuharakisha maendeleo ya Taifa na kuboresha ustawi wa jamii.

Taifa ambalo lipo nyuma kielimu, linakabiliwa na hali ngumu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Upo umuhimu mkubwa wa kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wananchi, inakuwa bora na inakidhi mahitaji ya jamii husika.

Ni wajibu wa Serikali na wadau wa sekta hiyo, kushirikiana katika harakati za kuiwezesha jamii kubwa kupata elimu.

Ukweli ni kwamba, nchi nyingi zilizopiga hatua ya maendeleo, ziliona umuhimu wa kuwekeza katika elimu iliyojaa maarifa, uwezo mkubwa wa kufikiri, ubunifu, ujuzi, ufundi wa aina mbalimbali na kuvumbua dhana mpya.

Sisi tunasema kuwa, hiyo ndio nguvu ya elimu inayoleta maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla. Wafadhili wametoa pesa nyingi kusaidia nchi maskini kama Tanzania lakini bado umaskini upo.

Jamii kubwa ya Watanzania inaishia katika lindi la matatizo ambayo nchi nyingi waliyatatua miongo kadhaa iliyopita. Wenzetu hivi sasa wanatafuta maarifa mapya ya kuibadili dunia wapendavyo kwa kurahisisha kila kitu kwa teknolojia na uvumbuzi mpya.

Imani yetu ni kwamba, suala la kuwekeza katika elimu bora haliepukiki bali linapaswa kutiliwa mkazo na kila mtu kwa kuzingatia umuhimu wake.

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema elimu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote duniani.

Zipo aina mbalimbali za elimu ambazo mtu anazihitaji ili aweze kuendesha maisha yake ya kila siku lakini elimu ya ufundi stadi ndio inayopewa kipaumbele zaidi na wananchi wengi ili waweze kujiajiri au kuajiriwa.

Elimu hiyo huwawezesha wananchi kusoma masomo ya maalumu katika vyuo mbalimbali vya ufundi stadi na kupata maarifa mapya.

Ili nchi yetu ipige hatua ya maendeleo, ipo haja ya kila mwananchi kuona umuhimu wa kusoma na kuelimika.

No comments:

Post a Comment