26 July 2012
Upelelezi kesi kesi ya Dkt. Ulimboka bado
Na Rehema Mohamed
UPANDE wa Mashtaka katika kesi ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari Dkt. Steven Ulimboka, umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Kesi hiyo ambayo inamkabili raia wa Kenya Bw. Joshua Mulundi (21) jana ililetwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Agnes Mchome.
Wakili wa serikali Bi. Mwanaisha Komba, alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo anaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa ambayo ni Agosti 7 mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Bw. Mulundi anadaiwa kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dkt. Ulimboka.
Katika shtaka la pili anadaiwa Juni 26 mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa Mwabepande Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha sheria alijaribu kumsababishia kifo Dkt. Ulimboka.
Kwa mara ya kwanza mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Julai 13 mwaka huu na kusomewa mashtaka yanayomkabili lakini hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, hadi itakapopelekwa Mahakama Kuu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment