20 July 2012

Ukaguzi leseni utapunguza ajali za barabarani nchini




Na Stella Aron

KUTOKANA na tatizo la ajira nchini, vijana wengi  wamefanikiwa kujiajiri katika uendeshaji wa pikipiki maarufu kama 'bodaboda' na kupunguza wimbi idadi ya wanaoshinda vijiweni na ukabaji.

Pamoja na kupungua kwa hayo yote bado kumekuwa na changamoto kubwa wanayokumbana nayo kutokana na wengi wa vijana hao kujiingiza katika fani hiyo bila kuwa na elimu.


Vijana wengi hawana elimu ya kutosha kuhusiana na suala zima la usalama barabarani licha ya kupunguza kero ya usafiri katika maeneo ya vijijini na mijini.

Kukosekana kwa ujuzi kumesababisha vijana wengi kupoteza maisha baada ya kugongwa na magari pindi wanapokuwa barabarani.

Kutokana na hali hiyo kumekuwa na changamoto kwa viongozi namna ya kuwawezesha vijana hao kupata elimu na hata kuwa na ujuzi ili kupunguza ajali za barabarani ambazo hivi sasa zimeshika kasi katika maeneo mengi nchini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Bw. Charles Kenyela amekiri kuwepo kwa idadi kubwa ya kesi zinazofikishwa vituoni kutokana na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda kugongwa na magari na wengine kupoteza maisha.

Anasema kuwa kutokana na changamoto hiyo wamelazimika kuanza kutoa mafunzo kwenye vituo vya pikipiki ili kupunguza ajali hizo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.

Anasema kuwa hivi sasa ni tofauti na zamani ambapo pikipiki zilizoeleka kufanya kazi kwenye ofisi mbalimbali na miradi ya maendeleo lakini kwa sasa ndiyo zimekuwa suluhisho la usafiri.

Kamanda Kenyela anasema kuwa, kuongezeka kwa pikipiki hizo kunatokana na kuingizwa na wafanyabiashara wakubwa kutoka katika nchi mbalimbali.

Anasema kuwa vijana wengi wamejikita kwenye biashara hiyo na kujikomboa kiuchumi lakini sasa biashara hiyo imeingia dosari kubwa kutokana na kushika nafasi ya kwanza kwa kuongoza kwa idadi ya majeruhi na vifo.

Takwimu za mwaka 2010, ninaonyesha kuwa zaidi ya watu 500 walifariki kwa ajali za pikipiki na wengine wengi kujeruhiwa.

"Hii ni hatari sana kama vijana hawa hawatapa elimu kwani tutakuwa na taifa lenye vijana wenye ulemavu na hata kupunguza idadi ya vijana, " alisema.

Anasema kuwa vijana wengi ambao wamejiingiza katika biashara hiyo hawana mafunzo wala leseni ya kuendeshea pikipiki hizo na hujifunza wanapokuwa kwenye vijiwe vyao tena kwa kubeba abiria.

Anasema kuwa, kutokana na hali hiyo jeshi hilo sasa limejikita katika utoaji wa elimu pamoja na ukaguzi wa leseni kwa waendesha pikipiki kama ilivyo kwa magari mengine.

Anasema kuwa kutokuwa na ujuzi wowote kumesababisha pia vitendo vya uporaji kufanyika mara kwa mara huku wahusika wakiibiwa mali hizo katika mazingira yenye utata.

"Kuna matukio mengi ya uhalifu ya pikipiki na mengine hayaripotiwi kutokana na wamiliki wao kutosajili vyombo hivyo jambo ambalo ni hatari, " anasema.

Anasema kuwa ili kuhakikisha kuwa madereva hao wanatii sheria za usalama barabarani polisi wa usalama hivi sasa wanawakagua madereva hao leseni, vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya usalama wa dereva na abiria wa pikipiki ambapo vifaa hivyo ni pamoja na kofia ngumu (helmet) mbili yaani ya dereva na abiria.

"Katika mkakati wetu wa kutoa elimu kwa madereva pia tumelazimika kutoa elimu kwa wanafunzi katika suala zima la kutii sheria bila kushurutishwa na kufahamu sheria za usalama barabarani, " anasema kamanda Kenyela.

Kamanda Kenyela anasema kuwa sababu kubwa inayochangia ajali hizo ni ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa kuwabebea abiria zaidi ya mmoja ili kupeleka hesabu kamili kwa matajiri.

Anasema kuwa ili kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawakua endelevu pia abiria wenyewe wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kukataa kupanda zaidi ya mmoja yaani maarufu kwa jina la mshikaki kwa wakati mmoja.

Anasema kuwa changamoto hizo zinapaswa kati ya abiria na serikali kwa kuweka sheria kali kwa waendesha pikipiki ili kudhibiti uvunjaji wa sheria wa mara kwa mara unaosababisha ajali.

Kamanda Kenyela anasema kuwa hivi sasa wameimarisha doria katika maeneo mengi ya jiji ili kupunguza ajali za pikipiki na matukio ya kihalifu yanayoendelea kutokea kwa katika maeneo mbalimbali.

Anasema kuwa sasa imefika wakati jamii ikabadilika kwa kufuata sheria bila ya kushurutishwa ambapo pia inaweza kupunguza kero ya madereva kushindwa kufuata sheria za usalama barabarani.

"Ili kupunguza suala hili jamii kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali tunapaswa kukemea suala la uvunjifu wa sheria za usalama barabarani kwa kutoa taarifa katika mamlaka husika, " anasema Kamanda Kenyela.

Anasema kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na skari wa usalama barabarani wamefanya kila jitihada za kuweka alama za usalama barabarani lakini baadhi ya madereva wanaovunja sheria hushindwa kufuata alama hizo na kusababisha ajali.

Hata hivyo Kamanda Kenyela amewashauri wamiliki wa pikipiki kuwaajili madereva wenye sifa na waliopitia mafunzo na si kuajili madereva wa vijiweni.

Aidha aliwashauri viongozi katika maegesho ya pikipiki nchini kuwa mfano wa kuigwa na hata kuweka msimamo wa kukemeana wao kwa wao pindi dereva anapobainika kuendesha mwendokasi unaohatarisha maisha ya watu.

"Madereva wanafahamina tabia hivyo itakuwa jambo la busara kama wataamua kukemea wao kwa wao nina imani kuwa hata ajali za barabarani zitapungua, " anasema.

Anasema jeshi hilo halitachoka kufanya ukaguzi wa leseni katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa kila dereva anatii sheria bila kushurutishwa.

No comments:

Post a Comment