03 July 2012

Twiga Stars yatoa la rohoni usagaji



Na Zahoro Mlanzi

TAARIFA za wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) kudaiwa kusagana, zimeichefua timu hiyo na kusema kwamba imedhalilishwa na kwamba haijawahi kutokea kitu kama hicho.

Kauli hiyo imekuja baada ya timu hiyo kuondoshwa katika kampeni ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWC) na Ethiopia.

Kuondolewa katika michuano hiyo, ilidaiwa kusababishwa na vitendo hivyo vilivyokuwa vikiendelea kwa muda mrefu ndani ya timu hiyo.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo Dar es Salaam jana, Meneja wa timu hiyo Furaha Francis, alisema wamesikitishwa na taarifa hizo zinazozidi kusambaa nchi nzima kwamba baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wanajihusisha na vitendo hivyo.

"Huwezi amini siku mbili nilishindwa kulala nikizitafakari taarifa hizo, tulitukanwa na baadhi ya mashabiki mara tu baada ya kumalizika kwa mechi yetu dhidi ya Ethiopia, kiukweli inanisikitisha sana," alisema Furaha.

Alisisitiza kwamba hakuna vitendo kama hivyo katika timu yake na kwa nini hayo yazungumzwe baada ya kufungwa na Ethiopia.

Alisema wamedhalilishwa juu na kauli hizo na kama kuna mtu kuna anachokijua ni bora watoe taarifa kwa viongozi, ili wajue ni jinsi gani watalitatua na si kusema pembeni.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake, Lina Mhando alisema hakufurahishwa na kauli hizo na kwamba wanajitahidi kurekebisha tabia ambazo ni kinyume na maadili kila kukicha, hivyo anashangazwa na kauli hizo.

"Tulikuwa kule Afrika Kusini wakati fulani wachezaji wa Algeria, Cameroon na Nigeria kiukweli kila mmoja alionekana tofauti katika kuvaa, hivyo sisi huku tunajitahidi sana katika suala hilo," alisema Lina.

No comments:

Post a Comment