03 July 2012
Swahili Fashion yawaangukia wadau
Na Amina Athumani
WAANDAAJI wa Jukwaa la maonesho ya mavazi ya nguo za kiswahili ya 'Swahili Fashion Week', wamewaomba wadau wa tasnia hiyo kuwafadhili ili kufanikisha jukwaa hilo kwa mwaka huu.
Jukwaa hilo limepangwa kufanyika Novemba mwaka huu, Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa jukwaa hilo ambaye ni mbunifu mkongwe wa mavazi nchini, Mustapha Hasanali alisema ugumu uliopo kwao ni kukosekana kwa wafadhili kuwapa sapoti.
Alisema maonesho hayo yamekuwa yakiibua wabunifu chipukizi kila mwaka na hiyo ni kutokana na kuwaandalia sehemu yao ya kuonesha mavazi pamoja na kushindania tuzo ya mbunifu bora chipukizi inayotolewa na jukwaa hilo.
Hasanali alisema kwa mwaka huu wanatarajia kutoa tuzo 20, tofauti na mwaka jana ambapo walitoa tuzo 17 na kwamba wameamua kuliboresha zaidi jukwaa hilo ili liweze kuwa na manufaa kwa kila atakayeshiriki.
Alisema kabla ya Swahili Fashion Week ya Tanzania wabunifu mbalimbali wa jukwaa hilo watashiriki Swahili Fashion Week Kenya, itakayofanyika Septemba mwaka huu ambapo amewataka wabunifu kuonesha nia ya kushiriki maonesho hayo, ili kukuza zaidi sanaa yao.
Mratibu huyo alisema wanategemea kupokea wabunifu kutoka nchi 15 za Afrika, ambao watashirikiana na wabunifu wa Tanzania katika maonesho hayo.
Alisema kwa upande wa Tanzania jumla ya wabunifu 21 wakongwe, watashiriki maonesho hayo huku chipukizi nao wakiendelea kujiandikisha kwa ajili ya maonesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka.
Mbunifu huyo alisema mara baada ya maonesho hayo, baadhi ya wabunifu watakaofanya vizuri katika Swahili Fashion Week watapata nafasi ya kuonesha mavazi yao kwenye nchi mbili za bara la Afrika na moja bara la Asia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment