10 July 2012

Tuangamize mazalia ya mbu kupambana na ugonjwa wa malaria



VITA dhidi ya Malaria iwe endelevu Kuangamiza mazalia ya mbu
kutaongeza ufanisi vita ya Malaria

SERIKALI pamoja na wadau wa sekta ya afya, imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kupambana na ugonjwa wa malaria ambao ni janga la kitaifa nchini na Afrika kwa ujumla.


Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinasema asilimia 85 ya wagonjwa wa malaria, wapo barani Afrika ambapo idadi hiyo imekuwa ikiongezeka Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ukweli ni kwamba, Tanzania haijafanikiwa kupunguza kasi ya ugonjwa huu kwa kiasi kinachotarajiwa bali imepunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Hatua hiyo imefikiwa kutokana na ongezeka la matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu kupitia mpango wa Serikali wa kuvigawa bure majumbani, katika Hospitali na Vituo vya Afya.

Vyandarua vingine vimekuwa vikiuzwa kwa gharamu nafuu maarufu kama 'Hati Punguzo'. 

Matumizi ya dawa mseto yenye uwezo wa kutibu ugonjwa huo kwa asilimia 95, nayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vinavyotokana na malaria.

Licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika vita hii, bado kuna changamoto mbalimbali zinazokwamisha ushindi kama ukosefu wa vituo vya afya vya Serikali ambavyo hutoa dawa mseto ambayo tunaambiwa ni tiba sahihi dhidi ya ugonjwa huo.

Sisi tunasema, umefika wakati wa Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi waishio vijijini.

Ifahamikie kuwa, ingawa kuna ongezeko la matumizi ya vyandarua vilivyotiwa viuatilifu, vyandarua hivyo humkinga mtu pale anapokuwa amelala tu lakini mbu aenezaye malaria, anaweza kumg'ata wakati wowote kabla ya kulala.

Maisha bora kwa kila Mtanzania, yanatakiwa kuzingatia uboreshaji wa afya ya msingi ili aweze kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa ufanisi na  kuongeza tija.

Serikali iwajibike kufikisha mpango wa kuangamiza mazalia ya mbu nchi nzima na kuufanya kuwa endelevu. Kwa kufanya hivyo, vita dhidi ya malaria itakuwa na mafanikio.


No comments:

Post a Comment