27 July 2012

SMZ yafungia meli 3 ikiwemo Seagull, Sepideh


Na Mwajuma Juma, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imezifutia usajili meli tatu kutofanya shughuli za usafiri ndani ya Zanzibar.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Bw. Abdallah Hussein Kombo, aliyasema hayo Malindi  jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.


Alisema uwamuzi huo umefanyika kutokana na uwezo wa mamlaka hiyo kisheria chini ya kifungu namba 17(1), cha sheria ya Usafri wa baharini visiwani humo.

Alizitaja meli hizo kuwa ni Mv Kalama, Seagull na Ms Sepideh ambazo ni chakavu na umri wa meli hizo kuwa mkubwa ambao hauimili tena harakati za bahari.

Aliongeza kuwa, kutokana na hatua hali hiyo wamiliki wa meli hizo watapatiwa hati maalumu ya kufungiwa meli zao ambapo baadae watatakiwa kupeleka vyeti walivyosajiliwa Zanzibar ili kupewa hati ya kuruhusiwa wazisafirishe nchi nyingine yoyote.

“Wamiliki wa meli hizi wamepewa muda wa mwezi mmoja kuziondosha na kusajili sehemu nyengine, mbali ya kuzifutia usajili, mamlaka yangu pia imeizuia meli ya Kilimanjaro III, isifanye safari zake kwa muda baada ya kubainika vyeti vyake vya usajili vimepitwa na wakati,” alisema Bw. Kombo.


Hata hivyo, alisema operesheni ya kukagua meli mbalimbali itaendelea hata zile ambazo zitaingizwa Zanzibar, zitakaguliwa na kama itabainika zina matatizo watazitoa.

Julai 18 mwaka huu, Zanzibar ilipatwa na msiba mkubwa baada ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit ambapo zaidi ya 100 walikufa na 146 waliokolewa waki hai.


Wakati huo huo, hadi kufikia jana maiti zilizoopolewa zimefiukia 123
 baada ya kupatikana kwa 17 na nyingine tano  kuzikwa
 kwenye fukwe za Pwani ya Bagamoyo, mkoani Pwani.


1 comment:

  1. walikua wapi siku zote mpaka maafa makubwa yanatokea ndio wanakagua meli. ni rushwa kila idara. watumishi wa serikali mshahara 300000 anamiliki mali ya bilioni 3

    ReplyDelete