19 July 2012

Simba yafufua matuimaini Kagame Cup *URA yatinga robo fainali


Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba jana walifufua matumaini katika michuano ya Kombe la Kagame, baada ya kuinyuka timu ya Ports ya Djibouti mabao 3-0 kwenye mechi iliyopigwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Hata hivyo Simba jana ilikuwa na uwezo kufunga mabao mengi kutokana na nafasi nyingi ilizozipata, lakini mshambuliaji wake Felix Sunzu alishindwa kuzitumia.

Katika mechi hiyo Simba, iliingia na uchu wa kutaka kufunga ambapo dakika ya pili Amri Kiemba, akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga alishindwa kufanya hivyo na badala yake kutoa pasi iliyokosa mmaliziaji.

Dakika ya 26, Simba ilikosa bao lingine baada ya Sunzu akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga alitoa pasi kwa Kiemba, ambaye alichelewa kuunasa mpira uliotoka nje.

Sunzu alikosa bao lingine dakika ya 36 baada ya kushindwa kuunganisha krosi safi ya iliyochongwa na Mwinyi Kazimoto.

Licha ya Simba kushambulia mfululizo, timu ya Ports ilionesha kandanda safi huku ikiwa imekamea mechi hiyo kutokana na wachezaji wake kukaba kwa jitihada kubwa.

Katika kipindi hicho timu hiyo ya Djibout, ilifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Simba lakini washambuliaji wake hawakuwa makini katika umaliziaji.

Kipindi cha pili Simba iliwatoa Amri Kiemba na Haruna Moshi 'Boban' na nafasi kuchukuliwa na Abdallah Juma na Uhuru Selemani.

Mabadiliko hayo yaliiongezea Simba nguvu ambapo dakika 46 Abdallah Juma, alikimbia na mpira huku akiwaacha mabeki na kupiga shuti kali lililookolewa na kipa.

Dakika ya 51 na 55, Sunzu alikosa mabao ya wazi akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga baada ya kubaki na kipa.

Juma aliipatia Simba bao la kwanza dakia 60, baada ya kuunganisha krosi ya Kazimoto ambaye jana alicheza wingi ya kulia.

Dakika ya 63 Simba ilipata bao la pili kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Sunzu. Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Denis Betes wa Uganda baada ya beki, Jean Niyobabariba kuushika mpira makusudi baada ya Kazimoto kumzungusha katika eneo la hatari.

Simba ilipata bao la tatu dakika ya 73 kupitia kwa Juma, kwa kichwa akiunganisha krosi ya Shomari Kapombe.  

Katika mechi iliyopigwa mchana ya michuano hiyo, URA iliifunga timu ya Vita ya jamhuri ya Kidemokraisi ya Congo (DRC), mabao 3-1 na kuifanya timu hiyo ya Uganda kupenya hatua ya robo fainali ikiwa na pointi sita.

No comments:

Post a Comment