16 July 2012

Polisi watoa tamko kwa CHADEMA



Na Salim Nyomolelo

JESHI la Polisi nchini, limesema halipo tayari kuwalazimisha viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili kuwahoji badala yake wataendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu kama zinavyotaka.


Msemaji wa jeshi hilo Makao Makuu Dar es Salaam, Bi. Advera Senso, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akijibu maswali ya mwandishi wa habari juu ya hatua ambazo watazichukua baada ya viongozi wa chama hicho kukataa kuhojiwa.

Alisema lengo la kutaka kuwahoji ni kuwapa viongozi hao msaada lakini kwa kuwa wamekataa kutoa ushirikiano, jeshi hilo haliwezi kuwalazimisha.

“Lengo letu ni kuwasaidia kutokana na malalamiko waliyotoa si vinginevyo lakini kwa kuwa wamekataa, sisi hatuwalazimishi badala yake tutaendelea kufanya kazi mwa mujibu wa sheria na taratibu za polisi kama zinavyotaka,” alisema Bi. Senso.

Aliongeza kuwa, licha ya viongozi hao kukataa kuhojiwa, upelelezi utaendelea kufanyika juu ya tuhuma walizotoa na kuwataka wananchi kufuata taratibu zilizopo wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.

“Ni kosa kwa mwananchi yeyote kutumia uvumi, maneno ya uongo, hisia au visingizio vyenye lengo la kuwazuia wengine kutoa maoni yao katika mchakato huu.

“Pia ni kosa kuhamasisha watu kuzomea, kukejeli au kutoa kashfa ili kumfanya mtu mwingine ashindwe kutoa maoni yake na kutumia lugha za vitisho wakati kwenye tume,” alisema Bi. Senso.

Juzi katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, alidai viongozi wa chama hicho hawapo tayari kuhojiwa na polisi juu ya madai waliyotoa kwa Serikali kutaka kuwateka na kuwadhuru.

Kutokana na madai hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliliagiza Jeshi la Polisi kuwahoji viongozi waliotoa tuhuma hizo ili wafanyie kazi madai hayo.

No comments:

Post a Comment