17 July 2012
NEEC kuwawezesha wajasiriamali wadogowadogo
Na. Mwali Ibrahim
SERIKALI imekuwa ikifanya jitihada za kuwezesha wananchi kiuchumi. Mikakati hiyo imekuwa ikianzia ngazi za chini hadi taifa.
Ili kufanikisha dhamira hiyo Serikali ilianzisha Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ili kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake.
Baraza hilo linasimamia utekelezaji wa sera ya Taifa ya uwezeshaji wananchi kwa kubuni, kupanga, kuratibu na kufuatilia shughuli zote za kuwezesha wananchi kiuchumi.
Kwa watu waliofika kwenye Maonesha ya 36 ya Biashara ya Kimataifa yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere na kutembelea banda la NEEC wanaweza kuwa mashuhuda jinsi baraza hilo linavyofanyakazi kubwa ya kuwezesha wananchi kiuchumi.
Katika maonesho hayo banda la NEEC liliibuka mshindi wa jumla hali inayodhihirisha kwamba NEEC imedhamiria kuhakikisha wananchi wanawezeshwa.
Akizungungumza na gazeti hili mara baada ya kutembelea banda la baraza hilo mmoja wa wananchi, Bw. Charles John, anasema bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali zina ubora unaokubalika, hivyo hakuna sababu ya kuendelea na utamaduni wa kuabudu bidhaa za nje.
"Nimeona jinsi wanavyozalisha samani zenye viwango na hata zaidi ya zile zinazotoka nje ninachoweza kusema NEEC imeishamaliza kazi yake kilichobaki ni sisi kuwaunga mikono kwa kununua bidhaa wanazozalisha," anasema Bw. John.
Anafafanua kuwa kazi kubwa ni kuwawezesha wajasiriamali hao kuwa na uwezo wa kuzalisha samani kwa wingi ili wakidhi mahitaji makubwa ya soko.
Alisema wajasiriamali wote waliokuwa kwenye banda la NEEC bidhaa zao zina ubora hivyo kinachotakiwa ni kuwaunga mkono. Mmoja wa washiriki wa maonesho hayo ambaye anatengeneza unga kwa kutumia, ndizi, Bi. Anna Kimambo ambaye ni mkrugenzi wa Kampuni ya Kishenga interprises anasema bidhaa zao kwa sasa zimekuwa kimbilio.
"Unga ninaotengeneza umekuwa kivutio na watu wengi waliofika kwenye banda hili wameonekana kuupenda," anasema.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo Mkurugenzi wa Uwezeshaji Dkt. Joyce Chonjo, anasema NEEC imetenga kiasi cha sh. bilioni 3 kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogowadogo kupitia katika vikundi vyao vya Kuweka na kukopa (SACCOS).
Anasema NEEC kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi itaendelea kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo kupitia Benki ya CRDB.
"Serikali imeshainia mkataba na Benki ya CRDB ambapo fedha za mikopo kwa wajasiriamali zitakazopitia katika benki hiyo itatoa mara tatu ya fedha hizo zikiwa ni mkopo kwa wajasiriamali, kwa mfano tutaweka sh. 1 bilioni, hivyo CRDB watatupatia sh. bilioni 3," anasema Dkt. Chonjo.
Dkt. Chonjo anasema mikopo hiyo inatolewa kwa mashariti ya riba isiyo zidi asilimia 15, ambapo CRDB hutoza riba ya asilimia 11 na vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) hutozwa riba kati ya asilimia moja na nne.
Anafafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 NEEC kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Baraza lilitumia sh. bilioni 7.4 kwa kuwawzesha wajasiriamali wadogowadogo katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Anataja mikoa 10 ambayo tayari imenufaika na fedha hizo kuwa ni Mtwara, Lindi, Ruvuma, Kigoma, Pwani, Singida, Dodoma, Tanga, Shinyanga na Rukwa. Anasema wajasiriamali 7,187 wamenufaika na fedha hizo.
Ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji na mikopo na Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na 16 ibara ya 16 (1) inaagiza kuanzishwa kwa mfuko wa uwezeshaji “ National Economic Empowerment Fund” ambao Baraza linauita Mwananchi Empowerment Fund, lengo likiwa ni Kumwezesha Mtanzania kuondokana na umaskini kwa njia ya kuongeza kipato pamoja na Kuhakikisha kuwa Watanzania wanamiliki uchumi wao.
Akizungumzia ushindi ambao NEEC ilipata Katibu Mtendaji wa NEEC, Dkt. Anacleti Kushuliza, anatoa mwito kwa Watanzania na Serikali kwa ujumla kununua bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali nchini, kwani zina ubora kiasi cha kushindana na zile zinazotoka nje ya nchi.
Anasema kwenye maonesho hayo baraza hilo liliwezesha wakilishwa wa kongano mbalimbali kushiriki, kuonesha na kuuza bidhaa zao.
Anasema walioshiriki ni pamoja na mafundi seremala ambao walionesha bidhaa wanazozalisha zenye ubora kiasi cha kuwavutia watu wengi.
"Hatuna sababu ya kuagiza samani kutoka nje na watu wengi waliofika kwenye maonesho hayo wamependa samani na bidhaa nyingine zinazozalishwa na wajasiriamali," anasema.
Anataja washiriki wengine waliowezeshwa na baraza kushiriki maonesho hayo kuwa ni wasindikaji wa vyakula, watoa huduma za vifungashio, watengenezaji na wabunifu wa nguo na wabunifu wa kazi za mikono. Anaeleza kuwa wote walikuwa wakionesha kazi zenye ubora.
Kuhusu majukumu ya baraza, Dkt. Kashuliza anasema baraza limeendelea kutimiza majukumu yake yaliyokusudiwa wakati wa uanzishwaji ikiwa ni pamoja na kuwezesha wananchi kiuchumi.
Anasema wananchi wengi wameendelea kutambua fursa za kiuchumi zinazowazunguka na kuzifanyia kazi. Eneo lingine ambalo baraza hilo limefanyia kazi kwa mujibu wa Dkt. Kashuliza ni uimarishaji na uudwaji wa SACCOS na VIKOBA.
Dkt. Kashuliza anasema NEEC imekuwa ikiratibu mafunzo ya wajasiriamali, mfano mafunzo ya ufundi seremala kutoka mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.
"Lengo la mafunzo haya ilikuwa ni kuwajengea uwezo mafundi hao ili waweze kutengeneza bidhaa bora zinazoweza kushindana katika masoko ndani na nje ya nchi," anasema Dkt. Kashuliza.
Kwa mujibu wa Dkt. Kashuliza mafunzo hayo yameleta matokeo mazuri, kwani yaliwezesha mafundi seremala shirikisho yao la TAWOFE. Aliongeza kuwa NEEC imekamilisha uundaji wa rasimu ya Mpango Mkkati wa Kisekta wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Anasema mpango huo utakamilishwa rasmi mwaka huu baada ya kupitiwa na wadau na kutoa maoni yao. Anafafanua zaidi kuwa baraza liliingia makubaliano na Taasisi ya Elimu ya taifa (TIE) ili kushirikiana katika kutengeneza mwongozo wa utoaji mafunzo ya wajasiriamali katika ngazi zote. Alisema kazi hiyo itakamilika kabla ya mwaka huu kumalizika.
Kuhusu changamoto, Dkt. Kushuliza anasema kumekuwepo na changamoto nyingi ambazo kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikikwamishwa au kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Baraza kama yalivyoanishwa kwenye sheria na mpango mkakati wa Baraza.
Changamoto hizo ni baraza kupata mgao wa fedha kidogo kupitia bajeti za kila mwaka za serikali, ambazo haukidhi mahitaji ya mpango.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment