04 July 2012
Mkutano Mkuu CHASHUBUTA Julai 7
Na Rose Itono
CHAMA cha Shule za Udereva nchini (CHASHUBUTA), kimewataka wamiliki wa shule hizo, kushiriki Mkutano Mkuu uliopangwa kufanyika Julai 7 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Katibu Msaidizi wa CHASHUBUTA ambaye pia Mkurugenzi wa Shule ya Udereva ya New Vision (VTC), Bw. Jonas Mhati, alisema lengo la mkutano huo ni kuchagua viongozi ambao watakiongoza chama hicho.
“Kwa mujibu wa katiba ya chama hiki, viongozi wanachaguliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu na watakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu, tunaomba wanachama wajitokeze kwa wingi.
“Mbali ya kuchagua viongozi, pia kutakuwa na mambo mbalimbali ya kujadili ili kuboresha utendaji kazi wa chama chetu,” alisema.
Bw. Mhati aliongeza kuwa, kitendo cha wanachama hao kukaa pamoja, kutatoa fursa ya kujadili changamoto mbalimbali, kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utendaji wa chama.
Alisema zipo changamoto nyingi ambazo hujitokeza kwa sasa ambapo ili kukabiliana nazo, ni wajibu wa kila mwanachama kutoka mikoa yote Tanzania Bara, kushiriki mkutano huo.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika Hoteli ya Crystol Palace, iliyopo Ilala Bungoni, kuanzia asubuhi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment