02 July 2012
Mashindano ya vishale yafunguliwa Mwanza
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MASHINDANO ya Wazi ya Vishale ya Afrika Mashariki yamefunguliwa rasmi juzi na Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Ajira na Michezo, Fenella Mukangara ambaye alipata ajali akielekea kwenye ufunguzi huo.
Akizungumza na wachezaji mjini hapa, Shelukindo alisema Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, imekuwa ikidhamini mashindani ya vishale kwa muda mrefu na kwa kutambua umuhimu wa mchezo huu kwa wapenzi na mashabiki itaendelea kudhamini mchezo huu katika mashindano mbalimbali ya ndani na yale ya kimataifa.
Alisema mchezo huo ni moja ya michezo ambayo inatakiwa ipewe kipaumbele kama michezo mingine na kwamba itafanyika jijini humo kwa siku nne ambayo yanashirikisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.
Alisema kampuni yao imetoa shilingi milioni 32 kwa ajili ya kugharimia mashindano hayo, ambapo pia watatoa medali pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya washindi wa kwanza hadi wanne.
Alisema pamoja na kudhamini mashindano hayo kwa mwaka wa tatu mfululizo, TBL pia imetoa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuchezea mchezo huo katika mashindano ya mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama cha mchezo (TADA), Gesase Waigama aliipongeza kampuni hiyo kutokana na kutoa udhamini mnono wa michuano hiyo ya Afrika mashariki mwaka huu.
Alisema mchezo huo unakabiliwa na tatizo la vifaa kuuzwa kwa bei ya juu na ni mara chache kwa mchezaji kuweza kununua vifaa hivyo, hivyo udhamni unaotolewa umekuwa ukiwakomboa wachezaji wa mchezo huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment