02 July 2012

Kocha Express amkubali Banahuzi



Na Neema Kalaliche

KOCHA Mkuu wa timu ya The Express ya Uganda, Charles Ayiekoh amekoshwa na kiwango kilichooneshwa na mshambuliaji mpya wa Yanga, Said Banahuzi kwa kusema ana sifa za kuwa mshambuliaji.

Timu hizo ziliumana Jumamosi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yote yalifungwa na Jeryson Tegete.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Ayiekoh alisema Yanga ilionesha kiwango kizuri kipindi cha kwanza lakini dakika 30 za mwisho ilionekana kutoelewana.

"Tunashukuru tumepata mazoezi ya kutosha katika mechi hii na unaona jinsi tulivyocheza, kipindi cha kwanza Yanga ilitusumbua na ndio maana wakapata mabao mawili," alisema na kuongeza;

"Lakini tuliporudi kipindi cha pili tulitulia kutokana na tulikuwa tayari tumeshaisoma na ndio maana tukafanya mashambulizi ya nguvu na tukapata bao moja ila mabeki hawakuweza kumkaba mshambuliaji wa Yanga aliyevaa jezi namba 11 (Banahuzi) ambaye alionekana kusumbua".

Alisema kikubwa ambacho mshambuliaji huyo anacho ni kuwa na nguvu na kutumia vizuri mwili wake kwani kila wakati huwasumbua mabeki.

Akizungumzia kiwango cha timu yake, alisema kila siku kinaongezeka na kwamba baada ya kumaliza ziara yao nchini ana imani kitakuwa katika nafasi nzuri ya kuanza msimu mpya wa ligi ya Uganda.

No comments:

Post a Comment