30 July 2012

Madiwani Shy wamtema Mwenyekiti halmashauri



Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WIMBI la kukataliwa kwa wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya na Majiji limeendelea kupamba moto baada ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kumuondoa madarakani Mwenyekiti wa Malmashauri hiyo Bw. Amos Mshandete.


Uamuzi huo ulifikiwa mwishoni mwa wiki kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani ambao walipiga kura za kutokuwa na imani na Bw. Mshandete ambaye ni Diwani wa Kata ya Ilola kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Bi. Mwajabu Abdalah, alisema hatua ya kukataliwa kwa Bw. Mshandete ilitokana na madiwani 24 kuandika barua na kuweka sahihi zao wakidai kutokuwa na imani naye hivyo kutaka aondolewe.

Alisema madiwani hao walimtuhumu Bw. Mshandete kwa kukiuka taratibu za uendeshaji halmashauri kwa mujibu wa kanuni zilizopo.

“Kura zilizopigwa katika kikao hiki zilikuwa 35 ambapo madiwani 25 walipiga kura ya kumkataa na tisa zilitaka aendelee na uongozi ambapo kura moja iliharibika,” alisema Bi. Abdalah.

Aliongeza kuwa, kutokana na matokeo hayo, Bw. Mshandete alitangazwa rasmi kuvuliwa wadhifa wa Uenyekiti wa halmashauri ya Wilaya hiyo ambapo nafasi yake itashikiliwa na Makamu Mwenyekiti.

Awali madiwani hao katika barua yao ya kutokuwa na imani na Bw. Mshandete walimtuhumu kukiuka miiko na maadili ya uongozi baada ya kubainika alikuwa akijipendelea katika suala zima la miradi ya maendeleo aliyokuwa akiielekezea kwenye kata yake.

Pia madiwani hao walimtuhumu Bw. Mshandete kutokana na tabia ya kutoa lugha chafu kwa baadhi ya madiwani hasa wakati wa vikao, kuwagawa madiwani kimakundi na kuchangia migogoro miongoni mwa watumishi wa halmashauri hiyo.

Tuhuma nyingine ni kuwachochea madiwani wanapokuwa ndani ya vikao vyao ambapo via vinahudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Ally Rufunga kudai posho kwa nguvu kukaida kusaini mkataba wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya zaidi ya miezi mitatu sasa.

Wiki iliyopita madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza walimwengua Meya wa jiji hilo Bw. Josephat Manyerere (CHADEMA) baada ya kumtuhumu kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka.

No comments:

Post a Comment