05 July 2012

Kilimo cha kisasa mpunga kuongeza uzalishaji



Na Radhia Ramadhani

BAADA ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, tumeendelea kushuhudia ongezeko la asasi mbalimbali za
kijamii zikijuhusisha na masuala ya kijamii na kiuchumi.

Baadhi ya asasi hizo zimeanzishwa nchi nzima na kusaidia jamii kuleta mawamko na uelewa wa haki zao za msingi.


Asasi zisizotambulika inatokana na utendaji wa
kazi mbovu ama kutojitangaza na kibaya zaidi kuna zingine zinaendesha mambo yake katika mikoba na hivyo kufifisha imani ya watanzania kuhusu wajibu wake.

Katika wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro asasi ya Dakawa Economic Development Organization, (DAKEDEO) ni maarufu katika kuwakomboa zaidi katika kilimo cha zao la mpunga.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa DAKEDEO, Bw.Amiri Msenga anasema ilianzishwa mwaka 2008 na kisha kupatiwa usajili wake wa kudumu mwaka 2010 na mpaka sasa ina wanachama kumi na tano.

Bw.Msenga anasema lengo la kuanzisha asasi hiyo ni kujenga, kuinua uchumi  na kuleta maendeleo ya wanachama na hatimaye ngazi ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Anasema, imejikita katika masuala ya mazingira, huduma za jamii, utamaduni, elimu na suala zima la ujasiriamali ambayo
kwa ujumla wake yakitiliwa mkazo ipasavyo yatasaidia kumuondolea Mtanzania umaskini.

Anasema katika kuhakikisha asasi hiyo inafanikiwa katika sekta hizo, imeuunda idara sita ndani ya asasi ambazo zitakuwa zikisimamia na kuratibu kwa ukaribu masuala yote yaliyoainishwa ili kuweza kupata mafanikio ya haraka kwa
wanachama na wakazi wote wa Wami Dakawa .

Anazitaja Idara hizo kuwa ni pamoja na Idara ya fedha na uongozi, mazingira na elimu, ujasiriamali, afya na huduma za jamii, mahusiano ya jamii na idara ya utamaduni
ambayo ndani yake kuna kikundi cha sanaa kinachotumika kuhamasisha na kupeleka ujumbe kwa wananchi kwa njia ya kuburudisha.

Bw.Msenga anasema tangu kuanzishwa kwa asasi hiyo imeshapata mafanikio ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufahamika na asasi zingine  zilizopo ndani ya wilaya ya Mvomero na nje ya wilaya.

“Katika hili kweli halina ubishi, wahenga walisema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, asasi yetu inazingatia usemi huu wa wahenga na ndiyo maana tumekuwa tukishirikiana na asasi mbalimbali kwenye miradi tofauti katika kuhakikisha
tunapiga hatua kimaendeleo,” anasema Bw.Msenga.

Anasema, hushirikiana na wadau wa mazingira katika suala zima la utunzaji wa mazingira ya milima ya Uluguru.

Anasema wamepata ardhi ya hekta arobaini 40 katika kijiji cha Mvumi, wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambayo
itatumika katika kilimo cha mazao mbalimbali kwa ajili ya kuwaongezea wanachama wake kipato na kuwainua kiuchumi.

Bw.Msenga anasema mafanikio mengine ni wanachama kumi na tano wa asasi hiyo kupatiwa elimu ya ujasiriamali kuhusiana na utengenezaji wa sabuni, vipodozi na dawa za aina mbalimbali za afya ya binadamu (kama za maumivu) kwa kutumia miti asilia.

Anasema ni jambo lisilopingika kuwa bidhaa nyingi zinazotengenezwa  kwa kutumia miti asilia hazina madhara katika mwili wa binadamu

Anasema wameweka mipango mikakati yake ya muda mfupi na
mrefu ambayo lengo lake kubwa na kuwawezesha zaidi kiuchumi wakazi wa eneo la Wami Dakawa.

Anaitaja mipango ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa wakulima wa miwa wa nje, ambao utaangalia jinsi ya kuwaweka pamoja na kuwasaidia katika ulimaji na kuvuna na kuzalisha sukari yao bila kutegemea kiwanda cha Mtibwa.

“Hili ni tatizo kubwa, mara nyingi utakuta miwa inayoanza kuvunwa ni ile ya kiwanda, ikimalizika ndiyo wanaangalia ya wakulima wa nje, ambao mara nyingi baadhi yao hujikuta miwa yao ikikataliwa kwa vigezo kuwa haikidhi ubora unaotakiwa na
matokeo yake mkulima huingia katika hasara kubwa, hii hali inabidi sasa kuimaliza,” anasisitiza.

Anasema katika kuhakikisha wanafanikiwa katika hilo watashirikiana na asasi ya ‘Building Africa Tanzania(chapter), BuATa yenye makao yake Kibaha, Pwani kwa
kuwawezesha kujenga viwanda vidogo vidogo vitakavyomilikiwa  na wakulima wenyewe.

Mpango mwingine kuweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia watu wa maeneo ya Kiroka, Kinole na Mkuyuni katika kuwahamasisha na kuwawezesha katika kilimo cha mazao ya viungo kama karafuu, mdalasini na pilipili manga.

Anasema wakazi wa hayo maeneo wanalima mazao hayo lakini si kwa kiwango kikubwa na bila mpangilio wa kilimo cha kisasa, hivyo imeona ni vyema kuwasaidia wakulima hao ili kilimo chao kiwe na tija zaidi kwa lengo la kuwainua kiuchumi.

Bw. Msenga anataja mpango mwingine kuwa ni kuboresha sekta ya ufugaji nyuki na kilimo cha alizeti katika maeneo ya Maharaka, Doma, Msongozi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji
zaidi kwa kutumia njia zilizo bora na hivyo kuwainua kiuchumi.

Anasema changamoto kubwa inayowakabili ni rasilimali fedha na uhaba wa nyezo ya kiutendaji.

"Uhaba wa fedha ndiyo changamoto kubwa, ingawa kuna baadhi ya wafadhili wachache kama kampuni ya sigara nchini TCC imeonesha dhamira ya kweli na ya dhati katika kuchangia kwa kiasi kikubwa katika masuala mbalimbali hususan suala la
mazingira," anasema.
 
Pia, bajeti ndogo ya kutekeleza mipango ya muda mfupi katika
asasi yao ni moja ya vikwazo vinavyochangia kuchelewesha kutoa huduma mbalimbali katika jamii inayowazunguka.

Naye mwanachama mwanzilishi katika asasi hiyo Bw.Prosper Mitti anatoa wito kwa watu mbalimbali na taasisi za kibenki kuzisaidia asasi zinazofanya kazi kwa karibu na wananchi kuhakikisha watanzania wanaondokana na umaskini.

             

No comments:

Post a Comment