10 July 2012
Dkt. Mwakyembe awakomesha madereva wa mabasi Ubungo
Na Anneth Kagenda
WAZIRI wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, jana alfajiri amefanya ziara ya kushtukiza katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani Ubungo, Dar es Salaam.
Lengo la ziara hiyo ni kujionea tatizo kubwa la upandishaji nauli kiholela na kuwataka madereva hao kutoa huduma kulingana na nauli zilizopangwa na kama hawataki, waache kazi mara moja na kwenda kulima viazi kijijini.
Baada ya kufika kituoni hapo, Dkt. Mwakyembe alisimama kwenye geti la kutokea mabasi hayo, kuingia ndani katika kila basi lililokuwa likitoka na kuwauliza abiria nauli walizolipa.
“Kama mnaona kazi mnayofanya ni ngumu, mnaweza kwenda kufanya kazi nyingine kama kulima viazi au kukata magogo badala ya kuendelea na kazi ambayo hamuiwezi.
“Hamuwezi kunyanyasa abiria alafu Serikali iwaangalie wakati sheria zipo, kwanini mpandishe nauli kiholela,” alisema.
Dkt. Mwakyemba ambaye aliongozana na Maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), aliwataka makondakta wa mabasi yote yaliyotoza nauli kubwa kwa abiria kuwarudishia pesa iliyoongezeka.
“Abiria leo nitatoa namba yangu ya simu ili mwananchi ambaye atatozwa nauli kubwa kwenye mabasi, anipigie ili nichukue hatua stahiki, huu ni utapeli, rudisha gari ndani mkawarudishie nauli zao na muwatoze nauli zilizopangwa na SUMATRA.
“Hatuwezi kuwafumbia macho wakati wananchi ndio wanaoumia, kila mtu aliyekutwa na kosa alipe faini kwa kila kosa sh. 250,000 na ikiwa mtu ataendelea kukaidi tutamfungia kutoa huduma,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake, Dkt. Mwakyembe alisema Watanzania wanafanyiwa madudu na baadhi ya madereva hivyo atahakikisha tabia hiyo inakomeshwa haraka iwezekanavyo.
“Hizi ni vurugu, madudu na utapeli kwa baadhi ya mabasi ambayo yanakwenda mikoa ya Kagera, Mwanza, Kigoma na Msoma, abiria wanalazimishwa kulipa nauli kubwa hata kama mtu hafiki mwisho wa safari, wengine leseni zimeisha muda wake, nimeamuru warudishiwe nauli zao.
“Mabasi yenye makosa yalipe faini kwa sheria za SUMATRA, kila kosa sh. 250,000, naona sekta ya Uchukuzi imeingiliwa na operesheni hii itakuwa endelevu,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliwataka SUMATRA kufanya kazi kwa kugawa muda wao nusu siku ofisini na uliobaki washughulikie tatizo hilo ndani ya miezi mitatu ili kukomesha tabia hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa SUMATRA, Bw. Ahmad Kilima, alisema wamefurahishwa na operesheni hiyo ambapo makosa mengi yanayahusu mabasi yanayotembea saa nane kuwa na dereva mmoja badala ya wawili.
“Si kwamba hatufanyi ukagusi hapana...Waziri alitaka kujiridhisha kwani mara nyingi huwa tunaangalia madaraja, kama tukibaini nauli zimepandishwa huwa mabasi husika yanalipishwa faini.
“Lengo ni kuhakikisha vitendo hivi havijirudii tena lakini jambo la msingi ni wananchi kutupa ushirikiano kwa maana ya kutoa taarifa ili tuweze kuchukua hatua,” alisema Bw. Kilima.
Baadhi ya magari yaliyokutwa na makosa ni yenye namba za usajiri T 707 BXZ Sumry, T 777 BCR, T 888 BUR, T 535 AJR la Mwanza, T 495 ATC ambayo tiketi zake zilikuwa za gari lingine.
Zingine ni TT 650 ALW linalokwenda Mwanza, T 308 AFU, T 689 BVM, T 333 BCX Sumry, T 448 BJE, T 491 AUF, T 442 XAZ ambayo leseni yake imeisha, T 685 BUW, T 620 BEW Sumry, T 658 BCT na T 285 EBQ.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment