23 July 2012
CECAFA yaridhishwa na viwango vya timu
Na Speciroza Joseph
KAMATI ya Mashindano ya Kombe la Kagame 2012, imeridhishwa na kiwango na nidhamu ilichooneshwa na timu zinazoshiriki michuano hiyo inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo, leo yanaingia hatua ya robo fainali, katika hatua ya makundi timu shiriki zilionesha kiwango kizuri na kushukuru mashabiki waliojitokeza kuangalia mashindano hayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicolaus Musonye alisema wameridhishwa na kumaliza hatua ya makundi katika hali ya usalama, huku kiwango na nidhamu kikiongezeka.
Alisema timu zote zimeonesha kiwango kizuri hadi kumaliza makundi ni mchezaji mmoja pekee aliyeoneshwa kadi nyekundu, hiyo imeongeza nidhamu ya mashindano tofauti na miaka iliyopita.
Musonye alisema mbali na nidhamu, mashindano ya mwaka huu yameanza vizuri kwa kuwa timu zote zimecheza kwa uwezo wao na kuingia hatua ya robo fainali.
Alizishukuru timu za El Salaam Wau ya Sudan Kusini, AS Ports ya Djibouti na Tusker FC ya Kenya zilizotolewa kwenye hatua ya makundi kwa ushiriki wao katika mashindano ya mwaka huu.
Musonye alizipongeza timu zote zilizoingia hatua ya robo fainali na kuzitaka zipambane zaidi na kuonesha viwango vyao hadi zitakapoingia fainali.
Alizitaja timu zilizoingia hatua ya robo fainali ambazo ni Simba SC, Yanga, Azam FC zote kutoka Tanzania Bara, Mafunzo ya Zanzibar, Atletico ya Burundi, APR ya Rwanda, AS Vita Club ya Congo DRC na URA ya Uganda.
Musonye alisema kutakuwa na mabadiliko ya ratiba endapo timu za Simba na Yanga, zitaingia nusu fainali kwa sababu za kiusalama.
"Kama Simba na Yanga zitavuka, nusu fainali ya kwanza itakuwa Jumatano na ya pili itakuwa Alhamisi kwa sababu za kiusalama kuwapa nafasi mashabiki wa timu hizo kuja uwanjani nyakati tofauti," alisema Musonye.
Musonye aliongeza kuwa kama timu hizo hazitaingia ama itaingia mojawapo, mechi za nusu fainali zote zitachezwa siku ya Alhamisi.
Alisema katika hatua ya robo fainali, nusu fainali na mshindi watatu hakutakuwa na dakika za nyongeza, kama timu zimetoshana nguvu zitapiga penalti za moja kwa moja, lakini mchezo wa fainali utakuwa na dakika 30 za nyongeza na penalti.
Hadi kumalizika hatua ya makundi jumla ya michezo 15 imechezwa, magoli 48 yamefungwa, ambapo mshambuliaji wa AS Vita ya Congo DRC anaongoza kwa kufunga magoli 5 akifuatiwa na Hamis Kiiza na Said Bahanuzi wenye magoli manne kila moja.
Fainali za mshindano hayo na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa siku Jumamosi kwenye Uwanja huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment