04 July 2012

Balozi Iddi: Tatizo la umeme nchini halitakuwepo tena


Na Gladness Mboma

SERIKALI imewahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara nchini kuwa, tatizo la kukatika kwa umeme halitakuwepo tena kutokana na mikakati madhubuti waliyonayo ya kuzalisha nishati hiyo wakitumia vyanzo mbalimbali pamoja na makaa ya mawe.


Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliyasema hayo jana wakati akifungua Maonesho ya 36 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Sabasaba.

“Taifa letu linakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa nishati ya umeme hivyo kukwamisha uzalishaji lakini Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuzalisha umeme kupitia vyanzo vyake mbalimbali ikiwemo makaa ya mawe,” alisema.

Aliongeza kuwa, maonesho ya mwaka huu yanakwenda sambamba na uoneshaji bidhaa kutoka nchini China ili kutambulisha ubora wake kwa Watanzania.

Balozi Iddi aliwataka Watanzania kuacha kuingiza bidhaa bandia nchini kwani hivi sasa Tanzania na China zimeingia makubaliano ya kushirikiana katika mambo mbalimbali.

“Tanzania imepewa nafasi kubwa ya kuuza bidhaa zaidi ya 400 nchini china bila ya kulipishwa kodi, kutokuwa na ukomo wa mauzo, tuchangamkie fursa hii ipasavyo,” alisema.

Alisema baadhi ya bidhaa ambazo huzalishwa nchini, hazina ubora unaotakiwa na kusababisha ongezeko la bidhaa bandia hivyo aliwataka wafanyabiashara kusindika bidhaa zao kabla ya kuchukua uamuzi wa kwenda kuziuza nje ya nchi.


1 comment:

  1. hizi hadithi zisizoisha tuu, kila mwaka wanasema hayohayo.

    ReplyDelete