01 June 2012

ZUKU yadhamini ZIFF kwa dola milioni moja



Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya ZUKU imedhamini Tamasha la Filamu la Kimataifa (ZIFF) kwa dola milioni
moja kwa miaka 10 kwa lengo la kusaidia kukuza filamu ambapo kwa mwaka huu
limepangwa kuanza Julai 7 mpaka 15, mwaka visiwani Zanzibar.

Akizungumza Dar es Salaam juzi usiku katika sherehe maalumu za kusherehekea kutimiza
miaka 15 tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo na kutangaza rasmi udhamini huo, Mwenyekiti wa Wanachi Group, Ali Mafuruki alisema lengo la kudhamini tamasha hilo kwa muda huo ni kuhakikisha wanalitangaza zaidi kimataifa huku wasanii husika wakinufaika nalo.

Alisema tamasha hilo litakuwa la aina yake kwa Afrika, kazi za wasanii hao watazitangaza duniani kote kupitia wasambazaji wao wa ZUKU Pay TV ambapo kwa hivi sasa wameenea katika Ukanda wa Afrika Mashariki na lengo lao ni kuenea zaidi.

Aliongeza kwamba anajua watu watakuwa na maswali mengi kwa nini wameamua kudhamini
ZIFF, hata hivyo alisema wameamua kufanya hivyo kutokana na sasa ni wakati wa wasanii kunufaika na kazi zao, kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakilia kutoona matunda ya kazi zao.

Alisema ni lazima wabadili dhana za wasanii hao kwa kuhakikisha wanafanya kazi zenye
ubora zaidi, ambapo zitasababisha kuwapa wao kiburi cha kuzidi kutangaza katika
mabara mengine.

Naye Mwenyekiti wa ZIFF, Mahmoud Thabit Kombo aliishukuru kampuni hiyo kwa udhamini
wao na kwamba ana imani mambo mazuri yatazidi kuja katika tamasha hilo kupitia kampuni hiyo.

Alisema huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano waliounzisha na kwamba wao ndiyo watakuwa
wadhamini wakuu, lakini watu wengine wanafunguliwa milango kudhamini tamasha hilo
kwani lengo ni kuhakikisha wasanii wanafaidika na kazi zao.

Mwenyekiti huyo alisema tamasha hilo lilikuwa linakabiliwa na changamoto nyingi hasa katika masoko, udhibiti wa hakimiliki ambapo kutokana na kuingia kwa ZUKU ana uhakika matatizo hayo
yatapungua.

No comments:

Post a Comment